LONDON, England
BAADA ya kuwa kocha wa Manchester United kwa muda wa
miaka 26, hatimaye wiki iliyopita, Sir Alex Ferguson aliamua kutangaza kwamba
anaachia ngazi.
Hadi anatangaza kuachia madaraka, Ferguson alikuwa
akitajwa kuwa ndiye kocha bora katika michuano ya Ligi Kuu ya England.
Hata hivyo pamoja na kuwa atakuwa akikumbukwa kwa
mengi, lakini utafiti uliofanyika inaonekana kwamba, pamoja na sifa
anazomwagiwa kwa suala la ushindi katika michuano ya Ligi Kuu ya England, yupo
nyuma kwa kocha wa zamani wa Chelsea ambaye kwa sasa anainoa timu ya Real
Madrid, Jose Mourinho.
Ifuatayo ni orodha ya makocha 10 katika michuano
hiyo na asilimia za ushindi walizonazo kwa sasa.
10. Kenny Dalglish - 48%
Nyota huyo wa zamani wa Liverpool, alianza kazi ya ukocha
katika klabu hiyo ya Anfield akiwa kocha mchezaji kazi ambayo alidumu nayo kwa
muda wa miaka sita kabla ya kustaafu mwaka 1991, baada ya kukusanya makombe 10
katika kipindi cha miaka sita.
Baada ya kuondoka katika timu hiyo, Dalglish alikwenda
kuinoa timu ya Blackburn Rovers ambako nako alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi
Kuu mwaka 1994.
Mwaka 1997, Dalglish aliteuliwa kuwa kocha wa timu ya
Newcastle United ambako alitumia muda wa
mwaka mmoja kabla ya kufukuzwa kutoka na matokeo yasiyoridhisha.
Mwisho Kenny alikwenda kuinoa timu ya Celtic, ambayo aliinoa
kwa muda wa miaka miwili na kuipa ubingwa Scotland kabla ya kurejea Liverpool
katika msimu wa 2011-12.
9. Andre Villas-Boas - 52%
Kabla ya kuanza kufundisha soka, AVB alifanya kazi chini ya
makocha vinara kama vile, Sir Bobby Robson na Jose Mourinho.
Villas-Boas aliacha kazi ya kuwa kocha msaidizi katika timu
ya FC Porto iliyokuwa chini ya Mourinho, na kisha kwenda katika timu ya
Academica ambako alikabidhiwa kibarua cha kuwa kocha mkuu.
Alipokabidhiwa timu hiyo aliweza kuitoa nafasi ya mwisho
kwenye msimamo wa ligi ambako timu hiyo ilikuwa haina ushindi na kisha
kuiwezesha kushika nafasi ya 11, huku ikiwa na pointi 10 kutoka kwenye mstari
wa kushuka daraja. Juni 2010, Andre Villas-Boas alirejea katika timu ya FC.
Porto na akiwa na timu hiyo kwa takribani miezi miwili aliweza kuchukua ubingwa
wa Kombe la Ureno na tangu aondoke FC
Porto, AVB ameweza kuzifundisha timu za
Chelsea na kwa sasa ndiye anayeinoa
Tottenham.
8. Claudio Ranieri - 52%
Kwa mara ya kwanza, Claudio Ranieri kutangazwa kuwa kocha ilikuwa ni mnamo mwaka
1986 akiwa na timu ya Lametini.
Hata hivyo baada ya muda wa miaka 14 baadaye alichaguliwa
kuwa kocha wa Chelsea.
Licha ya Ranieri kutotwaa ubingwa wowote akiwa na Blues,
lakini alijitengenezea jina nchini England, baada ya kuiongoza timu hiyo kwa
mechi 199 na kisha akashinda mechi 107 kati ya hizo kabla ya kwenda
kuzifundisha timu za Valencia, Juventus na kwa sasa ndiye kocha mkuu wa timu ya
Monaco.
7. Rafael Benitez - 55%
Benitez kwa mara ya kwanza kukabidhiwa kibarua cha ukocha,
alianzia katika timu ya Real Madrid B na
kisha kutimkia Liverpool mwaka 2004, baada ya kujiuzulu kuifundisha timu ya
Valencia.
Akiwa Liverpool, Benitez aliweza kutwaa mataji manne, kabla
ya mwaka 2010 kukimbilia Internazionale
na baadaye mwaka 2012 akarejea katika
soka la Uingereza akiwa kocha wa muda Chelsea.
6. Luiz Felipe Scolari – 56%
Scolari alikabidhiwa kibarua nchini England Julai 2008, alipochaguliwa kuwa kocha
wa Chelsea.
Kocha huyo ndiye wa kwanza kufundisha Ligi Kuu ya England,
akiwa ameshawahi kutwaa ubingwa wa Kombe
la Dunia, baada ya kutwaa taji hilo akiwa na Timu ya Taifa ya Brazil miaka sita nyuma.
Licha ya kupata mafanikio katika msimu wake wa kwanza,
Mbrazil huyo alitimuliwa kabla ya kufikia mwishoni mwa Februari, 2009 baada ya timu hiyo kufanya vibaya.
5. Arsene Wenger - 58%
Hadi sasa Arsene Wenger ni kocha wa Arsenal kwa muda wa
miaka 17 na katika kipindi hicho ameiwezesha klabu hiyo ya Kaskazini mwa Jiji
la London kutwaa mataji 11 na kati ya
mataji hayo mawili aliyapata katika msimu wake wa pili tangu aanze kuinoa timu
hiyo, wakati alipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA.
Licha Arsenal kutofahamika kutwaa ubingwa miaka ya hivi
karibuni tangu alipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2003-2004, lakini timu hiyo iliweza kushinda
mechi 38 bila kufungwa.
4. Roberto Mancini - 62%
Roberto Mancini aliteuliwa kuwa kocha wa Manchester City mwaka 2009, ikiwa ni baada ya
kufukuzwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mark Hughes.
Wakati anakabidhiwa timu hiyo alisaini mkataba wa miaka
mitatu na nusu na tangu kipindi hicho ameweza kufikia malengo kwa kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa
2011-2012.
3. Carlo Ancelotti - 63%
Carlo Ancelotti ndiye aliyechukua nafasi ya Guus Hiddink
akiwa kocha mkuu wa Chelsea FC Juni
2009.
Ikiwa ni takribani miezi miwili tangu, Ancelotti akabidhiwe
jukumu hilo aliweza kutwaa taji lake la kwanza wakati timu yake ilipoifunga
timu ya Sir Alex Ferguson, Manchester United katika mechi ya kuwania Ngao ya
Jamii, baada ya timu hizo kutoka sare ya 2-2 na kulazimu mshindi apatikane kwa
mikwaju ya penalti.
Mei 9, 2010, Muitaliano huyo aliweza kuiongoza Blues kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu na siku sita, baadaye akaiwezesha kutwaa Ubingwa wa Kombe
la FA, baada ya mechi ya fainali kuifunga Portsmouth bao 1-0.
Hata hivyo kwa bahati mbaya kiwango hicho hakikuonekana
msimu wa 2010-2011 na Ancelotti ikiwa ni
chini ya saa mbili tangu aifunge Everton akafukuzwa kazi.
2. Sir Alex Ferguson - 65%
Ingawa itawashangaza wengi, lakini ukweli ni kwamba Kocha
Sir Ferguson siyo bora katika michuano ya Lig Kuu ya England licha ya
kuitumikia kwa zaidi ya miaka 39.
Mscotland huyo kwa mara ya kwanza kutua Ligi Kuu ni pale
alipokabidhiwa jukumu la kuinoa Manchester United, baada ya kukabidhwa mikoba
ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Ron Atkinson mwaka 1986.
Mashetani hao Wekundu walitwaa taji lao la kwanza chini
ya Ferguson msimu wa 1992-1993 na tangu
kipindi hicho timu hiyo haijawahi kuonesha dalili za kushindwa kutwaa taji
hilo.
Katika kipindi chote ambacho, Sir Alex ameinoa timu hiyo,
ameweza kutwaa ubingwa wa Kombe la FA mara tano, Kombe la Ligi mara nne, Ngao
ya Jamii mara 10, Kombe la UEFA mara mbili, UEFA Super Cup mara moja, Kombe
la Intercontinental mara moja, Kombe la
Dunia kwa Klabu mara moja na Ubingwa wa Ligi Kuu ya England mara 13.
Hata hivyo pamoja na kutwaa mataji hayo, bado hakuweza
kupata asilimia kubwa ya ushindi katika michuano hiyo.
1. Jose Mourinho - 71%
Jose Mourinho (a.k.a, "The Special One") yeye
ndiye anayetajwa kuwa kocha bora kwa asilimia za ushindi katika historia ya
Ligi Kuu ya England, baada ya kujizolea asilimia 71% .
Mbali na hilo pia ni kocha wa sita wa Chelsea, kuingia
katika kumi bora.
Mourinho alijiunga na Chelsea akitokea FC Porto mwaka 2004.
Mreno huyo aliiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu
msimu wa 2004-2005 na 2005-2006 pamoja
na Kombe la Ligi mara moja na Ngao ya Jamii mara moja.
Msimu uliofuata kikosi hicho cha Mourinho, kilishindwa
kutwaa ubingwa huo kabla ya msimu wa mwisho kuiongoza klabu hiyo ya Stamford
Bridge, kutwaa ubingwa wa Kombe la FA na Kombe la Ligi na kisha Septemba 2007
akaitema klabu
hiyo.
Mbali na mataji hayo,
aliiwezesha Chelsea kutwaa Kombe la FA na Kombe la Ligi kwa mara ya pili kabla ya kuondoka Septemba
2007.
Mreno huyo hadi sasa ndiye anayetajwa kuwa na rekodi nzuri
ya ushindi katika michuano ya ligi hiyo.
No comments:
Post a Comment