Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, May 26, 2013

ALIKUWA NA MIGUU KAMA CHELEWA WAKADHANI ATAVUNJIKA LAKINI SASA......


MUNICH, Ujerumani
WACHEZAJI wa Real Madrid hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kushika magoti, viuno na vichwa wakihuzunika kufeli kutimiza ndoto yao ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, ambayo ilifanyika jana kwenye dimba la Wembley, jijini London.

Hilo la wachezaji wa Real Madrid lilitokea kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu - wakati ulipochezwa mchezo wa marudiano wa hatua ya nusu fainali baina ya wenyeji wa hapo, Los Blancos dhidi ya Wajerumani, Borussia Dortmund.

Real Madrid ilishinda 2-0, lakini kichapo cha mabao 4-1 walichokipata kwenye mchezo uliotangulia uliofanyika Signal Iduna Park, kilitosha kuitupa nje Los Blancos.
Lakini, wakati Robert Lewandowski anatoka zake ndani ya uwanja wa Bernabeu, aligundua kwamba rais wa klabu hiyo alipanga mpango wake fulani.

Akipita kwenye korido kuelekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, fowadi huyo wa Borussia Dortmund alijikuta akizuiwa na mtu maarufu kwenye mchezo huo wa soka na klabu ya Real Madrid, Florentino Perez. Perez hakuwa anakwenda, alisimama kumsubiri Lewandowski.

Akiwa amesimama kama mti na kumshangaa Lewandowski kama vile kitu cha ajabu, akajongea kwenye mlango uliopo kwenye eneo hilo alilokuwa amesimama na kuingia ndani. Mara walipoingia ndani, wawili hao waliketi kwenye meza na Perez hakutaka kuchelewesha muda kwa kwenda moja kwa moja kwenye mada.
Akamwambia Lewandowski: "Kama unaondoka Dortmund, kuna klabu moja tu unayopaswa kusaini kuichezea. Nataka uje hapa, kuongoza mashambulizi yetu msimu ujao. Naweza kukuthibitishia kwamba hutoweza kujutia."

Katika asubuhi ya tukio la baada ya Lewandowski kuisambaratisha Real Madrid kwenye mchezo huo wa nusu fainali, kulikuwa na stori pia kwamba kocha mtarajiwa wa Chelsea - Jose Mourinho alimtumia meseji staa huyo wa Poland, 24, kwamba waende kuungana pamoja Stamford Bridge.
Wakati ikiwa bado haijabainishwa wazi, maofisa wakuu ndani ya Bernabeu walithibitisha kwamba Perez amefanya mchakato wa kumvuta Lewandowski kwenye klabu yake ili kuitumikia timu hiyo. Kama hilo halitoshi, Lewandowski alionekana kutulia na kutumia zaidi ya dakika 15 kujadili jambo hilo na mtu huyo maarufu kwenye mchezo wa soka barani Ulaya.

Lakini, kwa Lewandowski Bayern Munich inabaki kuwa klabu ya chaguo lake, licha ya kwamba bado hakuna uhakika kama Dortmund itakubali kumwachia nyota wao mwingine aende akajiunge na mahasimu zao hao baada ya mwaka huu kumuuza Mario Gotze kwa pauni milioni 31.5.
Ukweli ni kwamba wanaweza wasikubali kumuuza fowadi wao huyo na kuwafanya Bayern wasubiri hadi miezi 12 ijayo kuwa mchezaji huru. Rais wa Real Madrid, Perez anamtaka Lewandowski ajiunge katika klabu yake, lakini Mourinho anaamini kwamba staa huyo atafiti zaidi kama atajiunga na Chelsea.

Kwa upande mwingine, Real Madrid, Bayern, Chelsea na Manchester United watamsubiri Lewandowski kuchukua uamuzi na hilo ndilo lililovuta hisia za wengi, wakati walipomkodolea macho mshambuliaji huyo wa Dortmund wakati usiku wa jana ilipomenyana na Bayern kwenye dimba la Wembley.
Lewandowski amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao manne kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa na kufanya hivyo dhidi ya timu kigogo kama Real Madrid, lakini mafanikio yake ndani ya Dortmund si kitu kinachoshangaza, hasa baada ya timu hiyo kuwa chini ya kocha Jurgen Klopp.

Kisera, Klopp amekuwa akiiga nyayo za Sir Alex Ferguson. Amekuwa akitumia muda mwingi kuwapeleleza wachezaji anaotaka kuwasajili kabla ya kufanya hivyo, zaidi ya hilo amekuwa akifuratia mazingira ya nyumbani ya kuwaandaa wachezaji wake.
Kwenye suala la nguvu, Lewandowski hakuzaliwa na nguvu hizo na kocha wake wa kikosi cha vijana cha timu ya UKS Varsovia Warszawa ya Poland.

"Miguu yake ilikuwa kama fimbo na siku zote alikuwa akiwatisha wenzake kwamba atavunjika muda wowote," alisema kocha huyo Krzysztof Sikorski.
"Siku zote nilikuwa na hofu kwamba atapata purukushani, kidogo inaweza kuwa tatizo, kwa sababu alikuwa mwembamba sana. Nilimtaka ahakikishe anaongezeka uzito na hapo akaanza kula vyakula vya kunenepesha. Kwenye hilo nilimpigia sana mkazo.

"Sikumzuia kuwa mfungaji bora. Nakumbuka msimu mmoja tulifunga mabao 158 na alifunga karibu nusu ya mabao hayo. Baadaye nilipata matumaini kwamba angekwenda kucheza Daraja la Kwanza Poland, lakini sikuwahi kufikiria kama angefunga mabao manne katika mechi dhidi ya Real Madrid kwenye mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya."

Mabao yake Varsovia yalimsaidia nafasi ya kuhamia KS Delta, na kupata mkataba wake wa kwanza wa soka la kulipwa, wakati alipokuwa akilipwa pauni 75 kwa wiki.
Hilo lilikuja baada ya uhamisho wake wa kwanza, ambapo Znicz Pruszkow waliilipa Delta pauni 1,000 na kumshuhudia fowadi huyo kuongoza kwa mabao katika mikikimikiki ya Ligi Daraja la Tatu na Ligi Daraja la Pili kwa msimu miwili mfululizo.

Kuifungia Poznan mabao 18 kwenye ligi na kuwasaidia kutwaa ubingwa jambo hilo lilimfanya Klopp kuanza kuvutiwa naye.
Rafiki wa Klopp alisema: "Jurgen ni mtu safi kwa wachezaji vijana. Ana umri wa miaka 45, lakini amekuwa akizungumza lugha yao. Si kwamba tu ni kocha, bali wamekuwa wakimchukulia kama rafiki, mtu ambaye wanamtegemea na mtu ambaye atasimama kuwatetea kwa chochote. Wanajifananisha naye.

"Kitu ambacho kilitokea Real Madrid kwa Jose Mourinho kumshusha kikosini Iker Casillas na kumgomea, kitu ambacho huwezi kufikiria kikatokea hapa. Jurgen amekuwa akiwaeleza kila kitu nyota wake mmoja mmoja na hakuna mchezaji aliyewahi kukumbana na maneno yake mabaya.

"Wakati Shinji Kagawa alipoondoka kwenda Manchester United, alilia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo mbele ya Klopp kwa karibu nusu saa. Kisha, Jurgen alimwambia: “Kwa nini asibaki kama atakuwa amekwazwa?”
"Kagawa alijibu kwamba hiyo ilikuwa nafasi adimu ambayo asingependa kuipoteza, lakini ukweli hakutaka kuondoka na hii inaonyesha bayana ni kwa jinsi gani kocha huyo anavyokubalika na wachezaji wake."

Kuhusu Lewandowski, ni mchezaji maarufu nchini Ujerumani na anayepamba vyombo vya habari. Anaendesha Mercedes, lakini yeye si mmoja wa wachezaji wanaolipwa fedha nyingi.
Fowadi huyo siku zote amekuwa msikivu na amekuwa akivaa mavazi ya kawaida tu na si mtu mwenye kuhamaki linapokuja suala la mjadala wa hatima yake ya miaka ijayo.

Uvumi wa kuhama na hatima ya maisha yake ya baadaye ya kisoka, umevuma kwa miezi 12, lakini fowadi huyo amekuwa mtulivu na kuendelea kufanya mambo ndani ya uwanja.
Kocha wa zamani wa Lewandowski katika klabu ya Poznan, lazima ataendelea kubaki mdomo wazi kutokana na kile kinachofanywa na mchezaji huyo.

No comments:

Post a Comment