MANCHESTER, England
ROBIN Van Persie ametua Manchester United na kuchagua kuvaa jezi yenye namba 20 mgongoni. Alipoulizwa, jibu lake lilikuwa rahisi tu, kwamba amechagua namba hiyo kwasababu timu yake hiyo mpya amehamia msimu huu ikiwa inasaka taji lake la 20 la England, hivyo anafanya hivyo kuwakilisha taji hilo.
Van Persie akatimiza hilo, kwa kuhakikisha anafunga mabao muhimu katika mechi muhimu na hatimaye klabu yake mpya ya Manchester United kufanikiwa kufanikiwa kutwaa taji lake la 20 la Ligi Kuu.
Mabao yake matatu 'hat-trick' dhidi ya Aston Villa katika mechi ya ushindi wa 3-0 kwenye dimba la Old Trafford juzi usiku, ulitosha kuipa United taji hilo la 20, lakini kubwa lililonogesha tukio hilo ni wachezaji wake wakishangilia kwa kuonyesha namba ya mgongoni ya Mdachi huyo baada ya mechi kumalizika.
Suala la mataji katika klabu ya Man United ni jambo linaloonekana kuwa rahisi kutwaa, lakini taji hilo la 20 limekuwa na historia ya aina yake kwa klabu hiyo na nyota wao huyo mpya, Van Persie, ambaye hilo lilikuwa taji lake la kwanza baada ya kusubiri kwa muda mrefu katika klabu yake ya Arsenal kabla ya kujiunga na Mashetani Wekundu hao wa Manchester.
Fowadi huyo wa Oranje, RVP alifurahia ushindi huo wa taji, lakini akibainisha masikitiko yake kutokana na kusubiri kwa muda mrefu sana kuweza kutimiza ndoto hiyo.
Kabla ya mechi hiyo, mitaani hakukuwa na shamrashamra sana za kuhusu ubingwa, zaidi ya maeneo ya karibu na Old Trafford ambapo 'wamachinga' walionekana kuuza bendera za timu hiyo, huku mashabiki wengine wakionekana kuvaa jezi zilizokuwa na namba 20 mgongoni na neno 'Champions', hivyo kwa Van Persie alikuwa na kila sababu ya kufurahia hiyo taji hilo kwasababu ni alama ya jezi yake.
Hofu kubwa ya mashabiki ilionekana kabla ya mchezo kuanza, ambapo walikuwa na wasiwasi kuona kama timu inaweza kutwaa ubingwa huo, hasa ukizingatia Jumatano iliyopita iliambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya West Ham United, walidhani kwamba Aston Villa nao wangetibua sherehe.
Licha ya kutawala mara nyingi, lakini United ilionekana kukosa ushawishi msimu huu kwamba ilikuwa na uwezo mkubwa wa kuwatesa wapinzani wao na hivyo hadi wanaifunga Aston Villa, jambo hilo lilikuwa na furaha kubwa kwa mashabiki wao.
Lakini, usiku huo wa mechi ulikuwa wa RVP, ukiacha kufunga mara tatu, Mdachi huyo alifunga bao maridadi kabisa 'volley', wakati alipounganisha pasi ya Wayne Rooney.
Na ndani ya nusu saa, tayari RVP alikuwa ametikisa nyavu mara tatu na kujihakikisha medali yake ya kwanza ya ubingwa kwenye shingo yake, huku mashabiki 75,591 waliokuwa wamefurika kwenye uwanja huo wa Old Trafford wakionekana kushusha pumzi na kuwehuka kwa mabao hayao yaliyowahihisha kuunyakua ubingwa huo.
Hofu ya mashabiki iliondoka kabisa baada ya kusikia sauti ya "Champions" ikitangazwa kwenye uwanja huo na kufurahia ushindi huo mtamu kabisa wa taji lao namba 20, ambapo linawaziba midomo wajirani zao "wanaopenda kuchonga", Manchester City.
Na hapo sherehe zikaanza, huku mashabiki wakionyesha mabango yao moja wapo lilisomoka hivi "Not nineteen forever".
MATAJI 20 YA UNITED
1907-8, 1910-11, 1951-52, 1955-56, 1956-57, 1964-65, 1966-67, 1992-93, 1993-94, 1995-96, 1996-97, 1998-99, 1999-2000, 2000-2001, 2002-03, 2006-07, 2007-08, 2008-09, 2010-11, 2012-13.
No comments:
Post a Comment