Mourinho akimpa maelekezo Xabi Alonso |
MUNICH, Ujerumani
KOCHA anayeamini uwezo wake, Jurgen Klopp wa Borussia Dortmund aliketi na MARCA saa 48 kabla ya mechi yake ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya dhidi ya Real Madrid.
Mechi hiyo, itafanyika leo kwenye dimba la Signal Iduna Park na kujiamini kabisa, Klopp anasema: "Sijaribu kumuiga mtu, mimi ni Klopp", alitoa kauli hiyo huku akicheka.
"Kwanini nisitabasamu wakati nina bahati? Ningependa kubainisha hapa, si kwamba sitabasamu, lakini ndio, nina furaha. Kazi yangu ni nzuri, nipo kwenye klabu nzuri na nina wachezaji mahiri.
"Real Madrid hawawezi kubadili staili yetu ya uchezaji, tutaingia uwanjani na kufurahia mchezo wetu. Ukweli ni kwamba timu nzuri sana kwa kucheza mashambulizi ya kushitukiza, kiwango chao hapo ni kikubwa.
"Kwenye hatua hii ya nusu fainali kuna timu tatu zinapewa nafasi - Real Madrid, Barcelona na Bayern. Kama ilivyokuwa mwaka jana. Sisi ni timu ya nne kwenye nusu fainali hii, kama Chelsea msimu uliopita. Na nani alishinda? Chelsea. Sisemi kesi yangu."
Lakini, hayo yakiwa ni maneno ya kocha, kipute cha leo, hakika kitakuwa na ushindani mkali, lakini kubwa linalotarajia hapo ni vita ya katikati ya uwanja, ambapo Xabi Alonso atakuwa kwenye kasheshe kubwa dhidi ya 'bwana mdogo', Ilkay Gündogan.
Hii ni vita inayotarajiwa kuwa na mvuto mkubwa kuitazama katika mchezo huo wa leo. Kiungo huyo kinda wa Kijerumani na veterani wa Kihispania watakuwa kwenye vita kubwa ndani ya dimba.
Wengi wanatarajia kuona makubwa kutoka kwa mchezaji huyo wa Borussia kama ilivyo kwa staa huyo wa Hispania, ambaye anatajwa kama mrithi wake katika kikosi hicho cha Real Madrid.
Alonso amekuwa mchezaji muhimu kabisa katika kikosi cha Jose Mourinho msimu huu licha ya kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara na wakati mwingine akilazimika kucheza akiwa na maumivu kama ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora dhidi ya Manchester United.
Kubadilika badilika ndani ya uwanja, pasi ndefu na ufundi wenye nidhamu kubwa uwanjani vitu hivyo vimekuwa vikifanywa na wachezaji wote hao wawili kwenye staili yao ya kiuchezaji.
Gündogan aliwasili Borussia kuziba pengo la Nuri Sahin, aliyepishana naye kuelekea Real Madrid.
Akiwa na umri wa miaka 22 tu, Mjerumani huyo, mwenye asili ya Uturuki, ana mambo mengi sana kwenye miguu yake kuliko matarajio ya wengi.
Na sasa jina la kiungo huyo limeanza kutajwa kwenye korido za uwanja wa Santiago Bernabéu kwamba huenda akawa usajili mpya utakaotua katika klabu hiyo.
Gundogan ni mmoja wa makinda bora kabisa barani Ulaya kwa sasa na haonekani kubweteka au kuvimba kichwa kutokana na mafanikio hayo. Kutokana na mazungumzo ya mkataba mpya wa Xabi Alonso kuwekwa kiporo kwa sasa, nusu fainali hiyo itakuwa nafasi ya muhimu kwa Gündogan kuonyesha thamani sahihi ya kiwango chake kiuchezaji.
Jambo hilo, ndilo linalofanya mchezo huo kuwa ni vita ya katikati ya uwanja, Alonso atakuwa kwenye kazi nzito ya kupambana na mtu, ambaye anayatajwa kama mrithi wake wa baadaye.
No comments:
Post a Comment