Javi Martínez akimruka Sergio Busquets kwenye mchezo wao wa juzi |
MUNICH, Ujerumani
BAYERN Munich
wameishushia Barcelona kipigo cha mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Allianz Arena,
juzi usiku kwenye nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mabingwa hao wapya
wa Bundesliga, walionyesha kiwango ambacho kinaingia kwenye historia na
kuiangushia kipigo cha mbwa mwizi Barca, ambayo inatajwa kama moja ya timu bora
zaidi duniani.
Tuchambue kiwango
cha Bayern.
Mfumo
Bayern waliingia
uwanjani wakitumia mfumo wa kujilinda wa 4-2-3-1, kuna wakati walikosa
mshambuliaji wa kweli, Barcelona wao walitumia mfumo wao wa kawaida wa 4-3-3.
Lionel Messi
alikuwa fiti kucheza, Mario Gomez alichukua nafasi ya Mario Mandzukic aliyekuwa
na adhabu na Arjen Robben alianza kulia. Jerome Boateng na Alexis Sanchez,
walianza kinyume na matarajio ya wengi kwenye timu zote mbili.
Mpango wa awali
Barca walianza kwa
kumiliki sehemu kubwa ya mchezo, wakipigiana pasi kwenye nusu yao, katika
harakati za kupima kasi ya Bayern.
Wajerumani hao
waliwaruhusu Gerard Pique na Marc Bartra kumiliki mpira na kujisahau, lakini
wachezaji wengine wote wa Barca walikabwa kwa karibu. Thomas Mueller
alitarajiwa kukaba mtu na mtu kwenye kiungo, lakini kazi yake ilibadilika na
kufunguka na kuwa huru.
Cha kufurahisha
alikuwa, Gomez ambaye alimkaba Sergio Busquets, mtu na mtu. Aliposhuka chini
sana alimuacha huru, alipovuka mstari tu na kuingia kwenye nusu ya Bayern,
Gomez alimuwahi na kucheza ‘man to man’.
Hili lilimfanya
Mueller kuongeza nguvu upande wa kulia wa uwanja, wakati Arjen Robben na Franck
Ribery walikuwa wakiwalinda mabeki wa pembeni.
Cha muhimu
kutambua hapa ni kuwa mfumo wa Bayern haukuwa ule wa ‘Man to man’ sana,
waliwazuga Barca ili wajione wanakabwa hivyo. Bayern walicheza karibu na adui zao
wakiwa na mpira, lakini ni wachezaji wachache sana waliokabwa kwa karibu.
Waliwalazimisha Barca kucheza kwenye eneo lao, wakati wao (Bayern) walikuwa
wakilinda pumzi zao kwa kuepuka kukimbizana na Barca.
Arrigo Sacchi amehusika
Hatari kubwa kwa
mfumo huu ni kwamba, Bayern walikabia juu sana, hasa kulinganisha na kasi ya
Sanchez, Messi na Pedro. Bayern walielekeza akili yao kwenye kuziba njia za
Barca kupitisha mipira, wakati kujipanga vizuri kwa Dante kulizuia mashambulizi
ya moja kwa moja kabla hata hayajaanza, staili hii ilikua ikitumiwa na kocha wa
zamani wa Italia, Arrigo Sacchi.
Javi Martinez
Kukabia juu, na
kupunguza kasi ya Busquets, iliwaruhusu Bayern kumfungulia mnyama wao, Javi
Martinez. Mhispaniola huyo wakati akiwa Athletic Bilbao alikuwa hana furaha
kila akikutana na Barca, lakini safari hii ameondoka na kiroho kwatu.
Alikuwa akipanda
mbele, akiwatia presha viungo wa Barca na kuwapandia kwenye enka zao usiku
kucha. Martinez alikaba mipira mara sita na kuingilia pasi mara mbili, kuna
wakati mwingine alipanda kusaidia mashambulizi, huku akiwa makini sana.
Bastian
Schweinsteiger alishuka chini kidogo wakati Martinez alipopanda mbele, wakati
jukumu la Mueller, lilimfanya wakati mwingine kushuka chini na kucheza sambamba
naye.
Kipindi cha pili
Martinez alipata
kadi ya njano sekunde ya 50 ya kipindi cha pili, baada ya hapo alipunguza kasi.
Ilikuwa faulo yake ya tano na alistahili kadi ya njano, hivyo mpango wa mechi
ulilazimika kubadilika.
Ni katika kipindi
hiki cha pili, ambapo faida ya kutokukimbizana na Barca inaonekana. Wachezaji
wa Bayern waliendelea kuonekana hawajachoka licha ya kufanikiwa kuwazuia Barca
katika kipindi cha kwanza, kitu ambacho timu nyingi hushindwa.
Wakati ambao Barca
walifanikiwa kuingia mchezoni na cha muhimu hapa kujua ni kuwa Barcelona
walifanikiwa kuanza kucheza vizuri baada ya Martinez kupata kadi ya njano.
Bayern wajikita
zaidi kwenye mfumo wa 4-2-3-1 (au 4-4-1-1, hasa ukiangalia jinsi ambavyo Franck
Ribery na Robben walivyokuwa wakishuka chini zaidi) na walitumia kiungo mkabaji
aliyekuwa akilinda mabeki.
Philipp Lahm
alimzidi ujanja, Jordi Alba kila walipokutana uso kwa uso pembeni ya uwanja na
Dante alikuwa na kiwango bora ambacho hutakuja kukiona tena kwa beki wa kati.
Mfumo wa mabeki wa
Bayern, ulikuwa sawa na ule uliotumiwa na AC Milan, lakini tofauti pekee
ilikuwa ubora na uzoefu. Robben alijituma bila kuchoka na alitisha, alianzisha
mashambulizi ya kushtukiza, aliingia na mpira ndani, kwa ufupi alikuwa vizuri.
AC Milan
walishindwa kutumia nafasi zao. Lakini Bayern walikuwa na uwezo wa kushinda
zaidi ya mabao manne.
Hitimisho
Barca hawakucheza
vizuri dhidi ya Paris Saint-Germain na Wafaransa hao walithibitisha kwamba beki
wa kati bora, stamina, nidhamu kwenye kiungo ndiyo vitu sahihi vya kuiua Barca.
Bayern walijumlisha
kujipanga kama Thiago Silva na Blaise Matuidi, walivyofanya, lakini Wajerumani
hao walikuwa na kitu kimoja cha ziada ambacho wote AC Milan na PSG walikosa.
Matokeo haya
yalikuwa yakuvutia sana, Barca walifunga mabao manne dhidi ya AC Milan, Camp
Nou, lakini ni ngumu kwao kufunga idadi hiyo ya mabao dhidi ya Mashine hizi za
Kijerumani.
No comments:
Post a Comment