MAISHA ya u-super star yana mambo mengi, watu maarufu
duniani wamekuwa wakikumbwa na mikasa mingi na zaidi mikasa ya kimahusiano
imekuwa mingi kiasi cha kuwachafulia kwenye masuala ya kijamii.
Kwa wanawake wenye umaarufu mara nyingi wamekuwa hawadumu
kwenye mahusiano, hata hapa nyumbani Tanzania mahusiano ya watu maarufu
yamekuwa kama ya kiti cha basi au gazeti
la mapokezi ambalo mtu yeyote ana haki ya kusoma.
Leo tunaangalia wanawake maarufu ambao wanaongoza kwa
kuolewa na kupigwa talaka mara kwa mara.
Kerry Katona |
Kerry Katona
Jina hili sio geni kwa wapenzi wa muziki wa R&B/Soul,
kwani aliwahi kutamba sana akiwa na kundi la muziki la Atomic Kitten.
Kerry, ambaye alishawahi kuwa mke wa mwanamuziki Bryan
McFadden kutoka kundi la Westlife, kwa sasa ni miongoni mwa nyota ambao leo hii
wanajumuishwa katika chama hiki cha mastaa waliozoea kuolewa na kuachika.
Baada ya kuachana na Bryan alijivunia kwa kupata ndoa
nyingine kwa Cabbie Mark Croft, hakudumu sana, aliachana naye na kisha hivi
karibuni kutangaza ndoa na mchezaji wa zamani wa mchezo wa Rugby, George Kay.
Angelina Jolie |
Angelina Jolie
Ukimchunguza Angelina Jolie unaweza kusema labda hafai kuwa
mwanachama wa chama hicho. Huyu ni miongoni mwa watakaopokea ahadi mpya na
kufunga pingu za maisha hivi karibuni tu.
Nyota huyo wa filamu nchini Marekani, Hollywood amekwisha
kumuahidi mpenzi wake wa muda mrefu, mcheza filamu Brad Pitt kuwa watafunga
ndoa mapema baada ya sheria ya mashoga kuoana kuhalalishwa kwenye Jimbo la
California, nchini Marekani.
Angie na Brad walianza mahusiano yao wakati wakiwa katika
kipindi cha utayarishaji wa filamu ya Mr & Mrs Smith, mwaka 2005, lakini
kumbukumbu zinaonyesha Angie aliwahi kuwa kwenye mahusiano na Jonny Lee Miller
mwaka 1994 na baadaye kufunga ndoa mwaka 1996.
Ukitaka kujua mapenzi ya Angie ni sanaa, wakati alipoolewa
alivaa fulana nyeupe iliyoandikwa jina Jonny kwa damu yake, ikiwa ni sehemu ya
kiapo cha mahusiano yao, ingawa hakuona aibu kung’ang’ania kuachika 1999, kisha
kuolewa na Jonny Lee Miller mwaka 2000.
Ulrika Jonsson
Masikini Ulrika ni aina ya mwanamke ambaye naye hajachoka
kujaribu kuwa kwenye mahusiano na mwanaume sahihi, ingawa kwa bahati mbaya
mapenzi yake huangukia kwa wanaume asioweza kudumu nao.
Mlimbwende huyo mwenye asili ya Sweden aliwahi kufunga pingu
za maisha na John Turnbull mwaka 1990 na ndoa kudumu kwa miaka mitano tu, hivyo
alifunga ndoa nyingine mwaka 2003 na mtangazaji kutoka kituo cha matangazo cha
MTV, Lance Gerrard-Wright.
Pengine nyota huyo (45) mwenye jumla ya watoto wanne na kila
mmojawapo akiwa na baba yake, ni mwepesi wa kusahau maumivu ya mapenzi, kwani
aliachana na Wright na kujitosa kwa kocha wa zamani wa England, Sven-Goran Erikkson,
ambaye ni mwenye sifa ya kutembea na vimwana mbalimbali duniani kwa mahusiano
ya muda mfupi na tena pasipo kujali utofauti wa umri.
Pamela Anderson |
Pamela Anderson
Ni ngumu kuitaja orodha ya wanachama wa chama hiki pasipo
kumtaja Pam, mcheza filamu mashuhuri aliyewahi kufunga ndoa na mpiga ngoma wa
bendi ya zamani ya “Motley Crue,” Tommy Lee, baada ya masaa 96 tu ya kujuana
kwao.
Faida ya ndoa yao ni kujirekodi mkanda wa ngono, kuzaa
watoto wawili kisha kumwagana mwaka 1998.
Mwaka 2006 alifunga ndoa ya pili na mwanamuziki Kid Rock,
ndoa iliyofanyika kwenye boti juu ya bahari ya Pacific kwenye fukwe ya St
Tropez.
Pengine hufahamu ndoa hiyo ilidumu kwa muda gani, yaani
ilikuwa mwaka mmoja tu, kwani Septemba 2007 alitangaza kuwa yupo kwenye
mahusiano na mtayarishaji wa filamu, Rick Salomon, ambaye baadaye mwaka huo huo
mwezi Desemba waliachana na kila mtu kuchukua maamuzi yake mengine.
Kate Winslet
Mcheza filamu huyo aliyekulia huko Reading Uingerza naye
amekwisha kuolewa mara tatu, kigezo kinachomfanya ajumuike kwenye klabu hii.
Mwanamume wake wa kwanza alikuwa muongozaji na mtayarishaji
wa filamu, Jim Threapleton, ambaye walianza mahusiano wakati wakiwa katika
maandalizi ya filamu ya Hideous Kinky, mwaka 1997.
Wawili hao walifunga ndoa mwaka 1998 na kupata mtoto mmoja,
lakini kutokana na umaarufu kuwa kiu yake, Kate alimbwaga Jim na kudondokea
kwenye mahusiano ya mtayarishaji maarufu, Sam Mendes ambaye alimtoa Uingereza
na kwenda kuishi naye New York.
Walifunga pingu za maisha huko Anguilla katika visiwa vya
Caribbean kipindi akiwa na ujauzito wa mtoto wake wa pili, Alfie. Mwaka juzi
Kate alidai talaka kutoka kwa Sam na sasa yumo katika ndoa na Ned Rocknroll,
ambapo inaelezwa kuwa ndoa yao ilifungwa kwa siri kubwa mwishoni mwa mwaka
jana.
Patsy Kensit
Nadhani kama chama hiki kitahitaji bingwa wao, bila shaka
mkanda wa taji hilo wangempatia Patsy, ambaye ameshakaa kwenye ndoa za wanaume
wanne hadi sasa.
Pengine muziki ndio chakula chake cha mapenzi, kwani
mwanandoa wake wa kwanza alikuwa muimbaji Dan Donovan, aliyefunga pingu naye
mwaka 1988, kisha muimbaji Jim Kerry aliyekula naye kiapo mwaka 1992.
Lakini kati ya wote hao, tunaamini mwanaume wake bora ni
Liam Gallagher, ambaye walidumu muda mrefu toka mwaka 1996 hadi mwaka 2007
walipokuja kufunga ndoa, na mahusiano yao yalikuja kuvunjika baada ya Liam
kutangaza kuwa aliwahi kumsaliti Patsy kwa kulala na Lisa Moorish kwenye wiki
ya kwanza baada ya kufunga ndoa yao, jambo lililopelekea Lisa kushika ujauzito
wa mtoto wake, Molly.
Dj Jeremy Healy ndiye mume wake wa nne, walioana mwaka 2010,
lakini mapenzi yao hayakudumu muda mrefu, kitendo kilichomfanya awe mwenye
kuchoshwa na kutokuwa na maisha ya ndoa kabisa.
Katie Price |
Katie Price
Ni ngumu kuwataja wanamitindo wenye mvuto wa kimahaba
duniani bila kumtaja Katie Price, maarufu kwa jina la Jordan.
Jordan ni chizi wa mapenzi, alianza kujulikana zaidi baada
ya kuwa kwenye mahusiano na mcheza mpira Dwight Yorke na baadaye muimbaji
Gareth Gates, muda mfupi baadaye alianza kuonekana na muimbaji raia wa
Australia, Peter Andre, ambaye walifunga ndoa mwaka 2005.
Walianza familia pamoja, huku Peter akibeba jukumu la kumlea
mtoto wa Yorke, Harvey kabla hawajazaa pamoja watoto wawili, Tiaamii na Junior.
Baada ya ndoa yao kuvunjika mwaka 2009 kwa madai kuwa Jordan
aliwahi kumsaliti Peter kwa kutembea na Leo Penna, alifunga ndoa nyingine na
Alex Reid mwaka 2010, ambayo ilivunjika mwaka huo huo.
Milionea huyo baada ya kukaa kwenye mahusiano mapya na
Kieran Hayler, ambaye ni mcheza shoo za uchi kwenye klabu ya usiku, hatimaye
wamefunga ndoa na kuna habari zimezagaa mitandaoni kuwa ni mjamzito.
No comments:
Post a Comment