Meneja wa Simba SC, Moses Basena, kipa Abel Dhaira na kiungo Mussa Mudde, wote raia wa Uganda, wamefukuzwa kwenye hoteli ya Spice, iliyopo Kariakoo, Dar es Salaam usiku huu kutokana na klabu hiyo kulimbikiza deni hadi kufikia Sh. Milioni 27.
Pamoja na kufukuzwa kwa Waganda hao, uongozi wa Spice Hoteli unashikilia magari mawili ya Simba SC, basi dogo na gari la kocha, aina ya GX110 hadi ulipwe fedha zake.
Kutokana na kufukuzwa Spice, Waganda hao walikwenda kuomba hifadhi katika hoteli ya Sapphire, ambako imeelezwa wamepokelewa na kupewa vyumba vitatu.
Kocha Mfaransa, Patrick Liewing pekee ameachwa aendelee kuishi katika hoteli ya Spice.
Mapema mchana wa leo, uongozi wa hoteli ya Sapphire Court, iliyopo Kariakoo pia, uliwazuia hotelini wachezaji wa Simba SC waliokuwa kambini hotelini hapo, ukishinikiza kulipwa deni la Sh. Milioni 25.7.
Simba SC ilizuiwa ikiwa inajiandaa kwenda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Hata hivyo, baadaye kaimu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itangare ‘Kinesi’ alikwenda kuzungumza na wamiliki wa hoteli hiyo na kufikia muafaka wa kulipa baada ya mechi ya Coastal.
Katibu wa Simba SC, Evodius Mtawala amesaini hati ya kuahidi kulipa deni hilo baada ya mechi ya leo na kuweka hati yake ya kusafiria kama bondi. Bado Menejimenti ya Sapphire inasistiza kulipwa fedha zake na kudai katibu wa Simba amekuwa akitoa ahadi hewa.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage yuko India kwa matibabu na Kinesi aliyeteuliwa kukaimu Umakamu Mwenyekiti, sasa ndiye anakaimu Uenyekiti wa klabu.
Aidha, Baraza la Wazee kwa pamoja na Baraza la Wadhamini, wameunda Kamati Maalum ya kusimamia timu kuhakikisha inafanya vizuri katika wakati huu mgumu, chini ya Mwenyekiti, Rahma Al Kharoos, maarufu kama Malkia wa Nyuki.
No comments:
Post a Comment