Kamati ya Rufani ya Uchaguzi
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeahidi wadau wa mchezo huo kuwa
itafanya kazi zake kwa misingi ya haki.
Akizungumza baada ya uzinduzi
wa Kamati hiyo uliofanywa Dar es Salaam leo mchana (Januari 23 mwaka huu) na
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kwa niaba ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga,
Mwenyekiti wa Kamati hiyo yenye wajumbe watano Idd Mtiginjola amesema wapo kwa
ajili ya kutenda haki.
Mtiginjola amesema Kamati yao
inaundwa na watu waadilifu, hivyo watafanya kazi kwa kuzingatia kanuni zilizopo
na sheria nyingine za mpira wa miguu ikiwemo Katiba husika.
“Niwakikishie kuwa hatutafanya
uamuzi kutokana na mawazo yetu, tufanya uamuzi kwa kuzingatia kanuni na sheria.
Kamati hii ni chombo cha haki, hivyo itafanya kazi zake kwa kuzingatia sheria.
Sheria na haki ni vitu viwili tofauti. Sheria zipo kwa ajili ya kuitafuta haki,”
amesema Mtiginjola ambaye kitaaluma ni Mwanasheria akiwa ni Wakili wa
Kujitegemea.
Baada ya uzinduzi, Osiah
aliwakabidhi wajumbe wa kamati hiyo vitendea kazi (instruments) mbalimbali
zikiwemo kanuni za uchaguzi za TFF na wanachama wake, Katiba ya TFF na Katiba ya
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Mbali ya Mtiginjola, wajumbe
wengine wanaounda kamati hiyo ni Makamu Mwenyekiti, Francis Kabwe ambaye ni
Naibu Msajili wa Mahakama Rufani ya Tanzania, Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mohamed
Mpinga ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria.
Mshambuliaji wa zamani wa timu
ya Reli Morogoro, Profesa Madundo Mtambo ambaye kwa sasa ni Mkufunzi katika Chuo
Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini Morogoro, na mdau wa soka
Murtaza Mangungu ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini.
No comments:
Post a Comment