SERIKALI
imepongeza wazo la kuanzishwa mbio za Uhuru Marathon ambazo zitakuwa
zikifanyika kila mwaka, lengo likiwa ni kudumisha umoja, amani na upendo
miongoni mwa Watanzania na kuenzi uhuru wetu.
Pongezi
hizo zilitolewa na Waziri wa habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk.
Fenella Mukangara wakati wa uzinduzi wa mbio hizo katika hafla
iliyofanyika kwenye hoteli ya JB Belmont jijini Dar es Salaam juzi
usiku.
Dk.
Mukangara alisema kuwa, kwa sasa kuna mbio nyingi za marathon hapa
nchini, lakini hakuna ambaye alikuja na wazo zuri la kuanzisha mbio kama
hizo za kuuenzi uhuru wetu na kudumisha amani nchini.
“Nawapongeza
waandaaji wa mbio hizi ambao ni vijana wa Kitanzania waliokuja na wazo
hili zuri la kuanzisha mbio za uhuru. Tunazo mbio nyingi sana hapa
nyumbani, lakini hatukuwa tumewaza kuanzisha mbio zinazolenga kuuenzi
uhuru wetu na kudumisha amani yetu.
Kwa niaba ya Serikali, napenda kusema wazi kuwa tumefurahishwa sana na
wazo hili la kuanzisha mbio hizi za uhuru na nichukue fursa hii kuwaomba
wadau na wapenda maendeleo ya michezo kuungana na taasisi hii
kufanikisha mpango huu ili uweze kuwa na mafanikio.
“Serikali
bado itaendelea kuweka miongozo na mazingira rafiki ya kushirikiana na
wadau wenye nia nzuri ya kuendeleza michezo nchini. Nina hakika
waheshimiwa mawaziri, wabunge, viongozi mbalimbali wa Serikali,
mashirika binafsi na viongozi wa dini wote watajitokeza kushiriki mbio
hizi,” alisema.
Awali
Mkurugenzi wa Kampuni ya Intellectuals Communications, Innocent
Melleck, walio waandaaji wa mbio hizo, alimuomba waziri afikishe ombi
lao kwa Rais Jakaya Kikwete kuwa mlezi wa mbio hizo.
Pia
walimkabidhi Dk. Mukangara fulana maalumu ya Rais Kikwete pamoja na ya
Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, kutokana na mchango wao
maalumu kwa mbio hizo.
“Mbali
na hilo tunapenda kuweka milango wazi kwa taasisi, kampuni na watu
mbalimbali kudhamini mbio hizo zenye malengo mazuri kwa Taifa,” alisema.
Mbio
hizo zinatarajiwa kuanza rasmi mwakani na zitakuwa zikifanyika kila
Desemba 8, kwa ushirikiano mkubwa wa Berlin Marathon na London Marathon.
No comments:
Post a Comment