Zaidi ya wanariadha 200 wamethibitisha kushiriki tamasha la mwaka huu la michezo la Karatu itakalofikia kilele chake Desemba 22.
Tamasha hilo la kila mwaka tayari
limekwishaanza, ambapo mechi za mpira wa miguu na michezo mingine
zinaendelea na zinatarajia kufikia tamati Desemba 21 kabla ya washindi
kukabidhiwa zawadi zao Desemba 22, siku ya ufungaji wa tamasha hilo.
Mratibu wa tamasha hilo, Meta Petro
amesema kuwa wanariadha zaidi ya 200 wameshajiandikisha kuahiriki
tamasha hilo, 160 wakiwa ni wanaume.
Amesema kuwa wanaume na wanawake
watachuana katika mbio za Km 10 wakati watoto wenye umri chini ya miaka
14 watapimana ubavu katika mbio za Kilometa tano.
Petro alizitaja baadhi ya timu
zilizothibitisha kuleta wanariadha wake katika tamasha hilo kuwa ni
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),
Majira Athletics Club, Hakika Wining Spirit, Guang ya Mbulu, Rift Valley
ya Karatu na klabu ya Babati huku Zanzibar utawakilishwa na klabu ya
Mukijope.
Mbali na riadha ambayo itafanyika siku
ya kilele cha tamasha hilo Desemba 22, mchezo mwingine ni mbio za
baiskeli ambao washiriki watachuana katika mbio za Km 60.
Amesema kuwa tayari waendesha baiskeli
33 wameshajiandikisha kushiriki katika mbio hizo na kwa upande wa mpira
wa wavu, timu ambazo tayari zimethibitisha kushiriki ni JKT Arusha,
Mbulu KKKT, Mbulu Wahame na Karatu Gypsum, ambao wataanza mbio za kusaka
ubingwa Desemba 20.
Amesema tamasha hilo ambalo hadi sasa
lina zaidi ya miaka 10 tangu lianzishwe lina lengo la kuibua na
kuviendeleza vipaji mbalimbali.
“Tuna mpango wa kuwasaka kina Filbert
Bayi wapya watakaochukua nafasi ya bingwa wazamani wa dunia wa mbio za M
1,500. Bayi ni mzaliwa wa Karatu na kupitia taasisi yake ya Filbert
Bayi Foundation na Olympic Solidarity pamoja na Kamati ya Olimpiki
Tanzania (TOC), amekuwa akiendesha tamasha hili la michezo na utamaduni
kila mwaka ili kuibua vipaji vipya na hali ya kupenda michezo kwa vijana
wa Karatu na Tanzania kwa ujumla,”.
No comments:
Post a Comment