Kikosi cha Yanga |
Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba 10 mwaka huu) ili kupitia
na kutoa uamuzi/ushauri kwa masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele
yake.
Wajumbe
sita kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti
Alex Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden
Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo.
Suala la ugombea wa Michael Wambura katika FAM
Michael
Wambura aliomba uongozi katika Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara
(FAM) katika uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana. Kamati ya Uchaguzi
ya TFF iliondoa jina lake kwa kukosa sifa ya kugombea nafasi hiyo.
Wambura
hakuridhika na uamuzi huo akapeleka shauri lake Kamati ya Nidhamu ya
TFF. Kamati hiyo katika uamuzi wake ilisema haina mamlaka ya
kushughulikia shauri hilo. Baadaye Wambura alikata rufani katika Kamati
ya Rufani ya TFF ambayo ilimpa haki ya kugombea.
Kutokana
na mkanganyiko huo wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwa na uamuzi wa
mwisho katika masuala ya uchaguzi ya wanachama wa TFF, na uamuzi wa
Kamati ya Rufani kuhusu uchaguzi wa mwanachama wa TFF, Sekretarieti ya
TFF iliomba mwongozo wa kisheria kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi
za Wachezaji.
Kwa
vile Kamati hizo mbili (Uchaguzi na Rufani) haziko katika mtiririko wa
moja kwa moja wa utoaji maamuzi, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji iliishauri Sekretarieti ya TFF kuliandikia Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ili kupata muongozo juu ya suala
hilo.
Katika
muongozo wake, FIFA ilitoa maoni kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF
chombo cha mwisho cha rufani katika masuala ya uchaguzi kwa wanachama wa
TFF ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF. Hata hivyo, FIFA ilishauri kuwa si
vizuri chombo kimoja kikawa msimamizi wa uchaguzi, na chenyewe tena
ndiyo kiwe cha mwisho katika uamuzi kwenye uchaguzi husika.
Hivyo,
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji imetoa mapendekezo
mawili kwenda Kamati ya Utendaji kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ili
kiwepo chombo kingine cha rufani pale mgombea anapopinga uamuzi wa
Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Mapendekezo
hayo ni; Iundwe Kamati ambayo itakuwa inasikiliza rufani zote
zinazotokana na uamuzi uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, hivyo
Kamati ya Uchaguzi ya TFF isiwe chombo cha mwisho cha uamuzi kwa rufani
zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF.
AU.
Rufani zote zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF zisikilizwe na
Kamati ya Rufani ya TFF. Kwa maana hiyo Kamati ya Rufani ya TFF ndiyo
kiwe chombo cha mwisho kwa wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati ya
Uchaguzi ya TFF kuwasilisha malalamiko yao.
USAJILI/PINGAMIZI DHIDI YA WACHEZAJI
Musa Hassan Mgosi, Ayoub Hassan Isiko
Mchezaji
Musa Hassan Mgosi ameombewa usajili Ruvu JKT kutoka DC Motema Pembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), na Ayoub Hassan Isiko ameombewa
usajili Mtibwa Sugar kutoka Bull FC ya Uganda. Wachezaji hao
hawaruhusiwi kuchezea timu hizo mpaka Hati zao za Uhamisho wa Kimataifa
(ITC) zitakapokuwa zimepatikana.
Toto dhidi ya Kagera Sugar kumsaini Enyinna Darlinton Ariwodo
Toto
Africans ilipinga usajili wa Enyinna Darlinton kwa timu ya Kagera Sugar
kwa vile bado ina mkataba wa mchezaji huyo ambao unamalizika mwakani.
Kwa
upande wake Kagera Sugar ilisema imemsaini mchezaji huyo kwa vile Toto
Africans imeshindwa kumlipa mshahara ambapo kuna makubaliano rasmi kati
ya Ariwodo kuwa klabu hiyo ikishindwa kumlipa mshahara anaruhusiwa
kuondoka.
Uamuzi
wa Kamati ni kuwa Ariwodo ni mchezaji halali wa Kagera Sugar kwa vile
Toto Africans ilishindwa kutimiza masharti ya mkataba.
Ramadhan Chombo ‘Redondo’
Redondo
ameidhinishwa kuchezea Simba kwa kuzingatia mchezo wa haki na uungwana
(Fair Play) baada ya klabu hiyo na ile ya Azam kufikia makubaliano
kuhusu mchezaji huyo.
Mchezaji David Luhende kusajiliwa Yanga
Yanga
ilikiri kutolipa ada ya uhamisho ya sh. milioni 5 kama walivyokubaliana
na Kagera Sugar. Awali waliipa Kagera Sugar hundi iliyogonga mwamba
benki (bounced cheque). Shauri hilo lilimalizwa kwa Yanga imetakiwa
kulipa fedha hizo ndani ya siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu.
Super Falcon dhidi ya Edward Christopher kusaini Simba
Simba
imepewa siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu iwe imeilipa Super Falcon
fedha za matunzo (compensation) kwa vile ndiyo iliyomlea mchezaji
Edward Christopher aliyesajiliwa katika klabu hiyo.
Toto Africans dhidi ya Mohamed Soud kusajiliwa Coastal Union
Toto
Africans iliweka pingamizi kwa maelezo kuwa bado ina mkataba na
mchezaji huyo. Hivyo kwa msingi wa Fair Play, mchezaji huyo
ameidhinishwa Coastal Union baada ya makubaliono kati ya klabu.
Rollingstone dhidi ya Kigi Makassy kusajiliwa Simba
Simba
imetakiwa kuilipa Rollingstone gharama za matunzo ilizoingia wakati
ikiwa na mchezaji huyo kwa kuzingatia kanuni za Shirikisho la Kimataifa
la Mpira wa Miguu (FIFA).
Super Falcon dhidi ya Sultan Juma Shija kusajiliwa Coastal Union
Uamuzi
wa Kamati ni kuwa Shija atachezea Coastal Union, na kwa vile yuko chini
ya umri wa miaka 23, Coastal Union itailipa Super Falcon fidia ya fedha
ilizotumia kumhudumia mchezaji huyo.
African Lyon dhidi ya Razak Khalfan kusaini Coastal
Lyon
imesema bado ina mkataba na mchezaji huyo. Kamati imebaini kuwa mkataba
wa mchezaji huyo na Lyon umemalizika, hivyo ni mchezaji halali wa
Coastal Union.
Flamingo dhidi ya Kelvin Friday kusajiliwa Azam
Friday
ruksa kucheza Azam, lakini klabu hiyo imepewa siku 21 kuanzia Septemba
10 mwaka huu kuilipa Flamingo gharama za kuvunja mkataba.
Super Falcon dhidi ya Robert Joseph Mkhotya kusaini African Lyon
Lyon
imeagizwa kuilipa Super Falcon sh. milioni moja ikiwa ni fidia ya
kuvunja mkataba wa mchezaji huyo ambaye imemsajili. Fedha hizo zitalipwa
kwa awamu nne kutokana na makato ya mlango yatakayofanywa na TFF.
Falcon itapokea malipo hayo kupitia TFF.
Oljoro JKT dhidi ya Othman Hassan kusajiliwa Coastal
Kwa
mujibu wa rekodi za TFF, mkataba wa mchezaji huyo na Oljoro JKT
unamalizika mwakani. Hivyo, Othman Hassan ni mchezaji halali wa Oljoro
JKT kwa vile bado ana mkataba na klabu hiyo.
Yanga dhidi ya Simba kuacha wachezaji wanne
Kamati
imetupa pingamizi hizo kwa vile hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa
wachezaji juu ya kuvunjiwa mikataba yao. Wachezaji hao walioachwa na
Simba ni Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiavanga na Lino Masombo.
Ikiwa
wachezaji hao watakuwa na malalamiko kuhusu kuvunjiwa mikataba suala
hilo litafikishwa katika Kamati kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa
uamuzi.
Mbuyu Twite
Kwa
mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa
Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Mbuyu
Twite, hivyo ni mchezaji wake halali. Hata hivyo, kwa vile Yanga imekiri
kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba na kukiri
kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku
21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
Kelvin Yondani
Kwa
mujibu wa Ibara ya 44(3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF,
Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kelvin Yondani, hivyo ni
mchezaji wake halali.
Kwa
vile Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu
yao, imetakiwa kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya
uthibitisho iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili
na Hadhi za Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa
madai/lalamiko husika.
Alex Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
No comments:
Post a Comment