WACHEZAJI 17 WAPINGWA KWENYE USAJILI
Klabu mbalimbali zimewasilisha
pingamizi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupinga usajili wa
wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu.
Toto Africans ya Mwanza imewawekea
pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na
Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na
wachezaji hao.
Pia Flamingo ya Arusha inapinga
usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii
(Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera
Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada
ya uhamisho haijalipwa.
Super Falcon ya Chanjamjawiri,
Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija,
Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma
Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali
za uhamisho hazikufuatwa.
Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa
usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu
hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass
Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba
hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri
wa miaka 23.
Azam inapinga usajili wa Ramadhan Chombo
‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11
mwakani. Nayo Simba inapinga Kelvin Yondani kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa
ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.
Vilevile Simba imewasilisha
malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko
Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele
yao, viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo
alilipwa dola 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake
ya kujiunga na klabu hiyo.
Nayo Yanga inapinga Simba kuwaacha
wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa
maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye
mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga
Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba
ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa
maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao
kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga,
Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
No comments:
Post a Comment