Watanzania wadhihirisha umoja Miss Grand International 2026



.Wambeba Jihan kwa kura za nchi yenye nguvu

Na Rahel Pallangyo

KATIKA moyo wa Afrika Mashariki kuna nchi ambayo historia yake inaishi katika mawe, bahari yake hubeba simulizi na asili yake husimulia hadithi ya kipekee na ya kuvutia.

Nchi hiyo ni Tanzania yenye urithi uliotukuka ambao ni hazina kubwa inayojumuisha watu wake adhimu, tamaduni tajiri na vivutio vya kipekee vya asili na kihistoria vinavyoifanya nchi kuwa ya kipekee duniani. 

Urithi huu umegawanyika katika makundi makuu mawili: Urithi wa watu (utamaduni na jamii) na urithi wa vitu (asili na majengo ya kihistoria).

Amani na umoja

Huu ni urithi mkubwa zaidi wa Watanzania. Licha ya kuwa na makabila zaidi ya 120, Tanzania imebaki kuwa kisiwa cha amani na mshikamano tangu kupata uhuru wake, shukrani kwa misingi thabiti ya waasisi wa taifa wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Lugha ya Kiswahili

Kiswahili ni urithi wa kipekee unaowaunganisha Watanzania wote. Ni lugha ya taifa inayotumika kama nembo ya utambulisho, utamaduni na kielelezo cha ukombozi wa Mwafrika ambayo sasa imekuwa lugha ya kimataifa.

Watu na makabila 

Jamii za Tanzania zina urithi wa kiasili unaovutia dunia nzima. Mfano mzuri ni jamii ya Wamasai na Wabarbaig ambao wameendelea kulinda utamaduni wao wa asili, pamoja na jamii za Wahadzabe na Wasandawe wanaoshi kwa kuwinda na kuokota matunda, wakiwa miongoni mwa wanadamu wa mwisho duniani wanaoishi maisha ya zama za kale.

Sanaa na burudani

Sanaa ya uchongaji wa vinyago vya shetani, muziki wa taarabu na ngoma za kiasili kama Sindimba na Bugobogobo ni sehemu muhimu ya utambulisho wa nchi.

Miss Grand Tanzania

Safari yetu ya kutazama urithi inaanzia Zanzibar, ambako nyumba za kale za Kiswahili, milango iliyochongwa kwa ustadi na kuta za mawe ya matumbawe zimehifadhi historia na utamaduni wa vizazi kwa vizazi. 

Zaidi ya hapo, fukwe zenye mchanga mweupe, maji safi yenye kung’aa, viumbe mbalimbali wa baharini na jahazi za jadi vinaakisi uzuri wa milele wa nchi yetu.

Lakini Tanzania ni zaidi ya pwani; katika nyanda pana za Serengeti, dunia ya wanyamapori huwa hai. Simba, tembo, twiga na aina nyingine nyingi za wanyama huzurura kwa uhuru, huku Uhamaji Mkuu wa Wanyama ukiikumbusha dunia nguvu ya ajabu ya asili. Hapa, safari si safari tu; ni kukutana na roho ya Afrika.



Lakini hadithi kubwa zaidi ya Tanzania haijaandikwa na maeneo pekee, imeandikwa na watu wake.

Pembeni yake wamesimama wanawake wawili wa Kimasai, wakiwa ni alama ya nguvu, ustahimilivu na ujasiri wa wanawake wa Tanzania ambao kwa vizazi vimejenga familia, jamii na mustakabali wa taifa.

Na katikati ya ubunifu huu unang’aa Tanzanite, hazina adimu inayopatikana Tanzania ikiwakilisha kina cha bahari zetu na upekee wa ardhi yetu.

Hilo si vazi tu, ni historia, ni utamaduni, ni watu, ni asili na ni Tanzania. Hivyo ndivyo Miss Grand Tanzania 2026, Jihan Dimack alivyoielezea Tanzania katika shindano la vazi la taifa kwenye mashindano ya kimataifa ya Miss Grand International 2026 juzi.

Katika shindano la Miss Grand International 2026 lililofanyika nchini Thailand, Jihan alionesha vazi la kitaifa lililopewa jina la ‘Fahari ya Nchi Yetu’ likiwa na ubunifu mkubwa uliolenga kutambulisha historia, utamaduni na utajiri wa maliasili za Tanzania katika jukwaa la kimataifa. 

Vazi hilo lilijumuisha pia maneno yaliyosomeka ‘PRIDE OF OUR HOMELAND’ (fahari ya nchi yetu), likiwa kielelezo kamili cha vivutio vikuu vya utalii, mazingira na asili ya Mtanzania. 

Jihan aling’ara kwa kuonesha umahiri wake katika kipengele hicho. Wakati akipita jukwaani kuonesha vazi hilo, alionesha kujiamini huku akitembelea kwa madaha mithili ya twiga, hali iliyozidisha urembo wake.

Kipengele cha nguvu ya nchi

Katika kipengele cha nguvu ya nchi kwenye mashindano ya Miss Grand International 2026, Jihan alianzia hatua ya kwanza kabisa ya mchujo.

Alianzia kwenye orodha ya nchi 50 za kwanza zilizotangazwa Septemba 27, 2026 ambapo Tanzania ilishika nafasi ya nane. Kutoka hapo, alipigiwa kura ili kuingia kwenye hatua ya nchi 40.

Aliendelea kuchanja mbuga kupitia kura za mashabiki kwenye mitandao ya kijamii, akavuka na kuingia hatua ya nane bora, kisha nne bora ambapo aliweka historia kama mwanamke wa kwanza Mwafrika kufika hatua hiyo na baadaye tatu bora.

Hivi sasa amefanikiwa kuingia hatua ya mwisho kabisa ambapo anachuana vikali na mwakilishi wa Ecuador, Shyare Andrade.

Mshindi wa kipengele hicho atapata nafasi ya moja kwa moja ya kuwa miongoni mwa warembo 20 bora wa shindano hilo linalofanyika Thailand na fainali zitafanyika kesho.

Nguvu ya mashabiki

Nguvu ya mashabiki wa Tanzania kwa Jihan katika shindano hili ni ya kihistoria na ya kuigwa mfano. Imethibitisha kuwa nguvu ya kura na mshikamo wa mitandaoni wa Watanzania unaweza kutikisa majukwaa makubwa ya urembo duniani, jambo lililokuwa chachu ya mafanikio yake makubwa.

Nguvu hii inajidhihirisha katika uongozi wa kura kimataifa.

Mashabiki wamemwezesha Jihan kutawala vipengele vikuu vinavyotegemea kura. Kwenye kipengele cha nguvu ya nchi Tanzania ilifikia asilimia 48 ya kura zote, ikiongoza dhidi ya nchi zenye nguvu kubwa ya mashabiki wa urembo kama Ecuador na Vietnam.

Mbali na nguvu ya nchi, mashabiki wamempa Jihan uongozi wa asilimia 35 kwenye kura za Miss Popular, kielelezo tosha cha jinsi anavyopendwa na kuungwa mkono kwa dhati.

Kupitia ushirikiano wa mashabiki wanaoshirikiana kusambaza, kupenda, kupandisha tena na kuwakaribisha wengine kupiga kura, Jihan amekuwa mwanamke wa kwanza kutoka Ukanda wa Afrika kufika hatua ya mbali zaidi kwenye kipengele cha nguvu ya nchi ya mwaka.

Nguvu hii ya mashabiki imeipa Tanzania heshima kubwa na kuonesha kuwa nchi ina ushawishi mkubwa pindi inapoungana kuunga mkono wawakilishi wake kwenye anga za kimataifa. 

Jihan ni nani?



Jihan anasema anajivunia kuwa nusu Mtanzania na nusu Mlebanon na kuwa mwanamke wa tamaduni mbili kumempa mtazamo wa kipekee kuhusu ulimwengu. 

“Nimejifunza kuthamini mila tofauti, kuelewa njia tofauti za maisha na muhimu zaidi, kutambua uzuri katika utofauti wetu,” anasema.

Ameishi Tanzania, Lebanon na Msumbiji na kwa sasa anafanya kazi nchini China ambako amejijengea uzoefu katika uanamitindo, biashara na masoko.

Safari yake ya uanamitindo ilianza akiwa na umri mdogo wa miaka 17 tu na ndipo alipoanza kufanya kazi na kujifunza thamani ya kujitegemea, nidhamu na wajibu. 

Safari yake kwenye urembo imekuwa sehemu ya pekee katika maisha yake, kwani ameshiriki katika mashindano mbalimbali, ikiwemo Miss Tanzania. 

Ingawa hakuchukua taji lilimfundisha somo muhimu kuhusu uvumilivu, uthabiti na kujiamini.

“Mwaka 2016 nilipata bahati ya kushiriki Miss Universe Tanzania ambapo nilibahatika kutwaa taji hilo na kuiwakilisha nchi yangu nzuri kwenye jukwaa la Miss Universe,” anasema.

Uzoefu huo ulimpa fursa ya kuona ulimwengu, kukutana na watu na kuelewa wajibu na kubeba jina la nchi nje ya mipaka yake.

“Sasa nimebarikiwa kupata nafasi nyingine ya kuiwakilisha Tanzania, safari hii nikiwa Miss Grand Tanzania 2026 nchini Thailand. Kwangu hii ni zaidi ya taji nyingine, ni fursa ya kuuonesha ulimwengu Tanzania ni nani... Ninataka kuonesha utamaduni wetu, utofauti wetu, uchangamfu wetu na uelewa wetu wa watu tofauti na tamaduni tofauti. Ninataka kudhihirisha maana ya kuongoza na kuwa balozi wa kweli wa nchi yangu,” anasema Jihan.

Anaongeza: “Tanzania inajulikana sio tu kwa mandhari yake ya kuvutia na mbuga za kitaifa zenye kupendeza, bali kwa amani yake, umoja na maelewano. Haya ni maadili ninayobeba popote ninapokwenda.

Nataka watu waione Tanzania inayosherehekea tofauti, inayokumbatia utofauti na kuchagua amani.

Leo, ninasimama mbele yako kama mwanamke aliyeundwa na tamaduni tofauti, nchi tofauti, uzoefu tofauti na sura tofauti za maisha yangu.

Mtanzania kwa moyo, Mlebanon kwa urithi, umbo la kimataifa na utofauti wa fahari.

Mimi ni Jihan Dimack, niko tayari kubeba hadithi ya nchi yangu kwa ulimwengu kwa tabia, kwa kusudi na kwa amani,” anasema.

Acha vita na vurugu

Anasema kampeni yake ya  ‘Acha Vita na Vurugu’ inawakilisha wito wa ubinadamu, amani, uvumilivu na heshima. 

Anasema vurugu hutenganisha au huharibu familia, jamii, fursa na matumaini ya vizazi vijavyo. “Ninaamini kwamba amani ya kudumu huanza na jinsi tunavyotendeana kwa uelewano, mazungumzo, huruma na heshima kwa utu wa binadamu,” anaeleza.

Anaongeza: “Kama Miss Grand Tanzania 2026, nataka kutumia sauti yangu kuwahimiza vijana kukataa vurugu na kuwa mabalozi wa amani katika nyumba zao, jamii na ninaamini kwamba kuchagua mazungumzo wakati wa migogoro na kuwa na huruma na kuacha chuki ni mojawapo ya njia zenye nguvu zaidi. Tunaweza kuchangia ulimwengu wa amani zaidi”.

HABARI HII ILITOKA MARA YA KWANZA HABARILEO

No comments