MELI YAWAKA MOTO ZIWA NYASA NA KUUA WATATU
Watu watatu wamefariki dunia na wengine zaidi ya 40 wameokolewa baada ya meli ya MV Chambo, iliyosajiliwa nchini Msumbiji, kuwaka moto ikiwa katika safari zake kwenye maji ya Ziwa Nyasa kutoka Tanzania kuelekea Msumbiji.
Kwa mujibu wa taarifa meli hiyo ilikuwa imetoka bandari ya Mbambabay.
Ajali hiyo ilitokea Jumapili ya Oktoba 11, 2026, majira ya saa 10:30 alfajiri katika eneo la Chiulu wilayani Nyasa, wakati chombo hicho kikiwa kimebeba jumla ya abiria 44 pamoja na tani 10 za mizigo.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mheshimiwa Peresi Magiri, amebainisha kuwa waliokuwamo ndani ya meli hiyo ya Msumbiji ni raia 23 wa Msumbiji, 15 wa Tanzania, wanne wa Malawi pamoja na raia wawili wa Lesotho.
Waliofariki dunia katika mkasa huo ni mtoto wa kike raia wa Msumbiji, mwanamke raia wa Malawi, na Mtanzania Yuston Chatanda ambaye ni mkazi wa Nombe, huku watu wote waliookolewa wakipatiwa msaada unaostahili.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea na operesheni katika eneo hilo, huku DC Magiri akithibitisha kuwepo kwa mawasiliano na Msumbiji na Malawi, ambapo Msumbiji tayari imetuma boti kuchukua mwili wa raia wake wakati uchunguzi wa chanzo cha moto ukiendelea.
Post a Comment