Mafuru Ataja Fursa za Kibiashara na Uchumi Mwanza


Wafanyabiashara, wawekezaji na wazalishaji wa bidhaa nchini wametakiwa kuchangamkia fursa za kimkakati zilizopo mkoani Mwanza ili kuongeza thamani ya bidhaa, kukuza biashara na kupenya kwenye masoko ya ndani, kikanda na kimataifa. 

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Ephraim Mafuru, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Manispaa ya Ilemela kando ya Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF-2026).

Mafuru alisisitiza kuwa mkoa huo una nafasi kubwa ya kugeuka kuwa kitovu kikuu cha biashara katika Kanda ya Ziwa na ukanda mzima wa Afrika Mashariki kutokana na mchango wake mkubwa kiuchumi, uwepo wa Ziwa Victoria na uboreshaji wa miundombinu.

Akieleza takwimu za mchango wa kiuchumi, Mafuru alibainisha kuwa Jiji la Mwanza pekee lilichangia kiasi cha Shilingi trilioni 14.8 katika Pato la Taifa (GDP) kwa mwaka 2025, kiasi kinachowakilisha takriban asilimia 7.2 ya GDP yote ya Tanzania, ambapo mafanikio haya yanatokana na shughuli mbalimbali ikiwemo biashara, viwanda, uvuvi, kilimo, ufugaji na uchimbaji wa madini. 

Kufuatia ukuaji huo, alisisitiza kuwa uzalishaji hautakiwi kuishia katika kuuza bidhaa za asili au ghafi, bali wadau wanapaswa kuelekeza nguvu zao kwenye uwekezaji wa kusindika, kufungasha, kuhifadhi, kutumia teknolojia ya kisasa, kuboresha usafirishaji na kutumia masoko ya kidijiti ili kukidhi viwango vya ushindani vya kimataifa.

Aidha, Mafuru aliongeza kuwa nafasi ya kijiografia ya Mwanza kandokando ya Ziwa Victoria inaipa faida kubwa ya kiushindani katika kurahisisha usafirishaji na kuunganisha mitandao ya kibiashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Afrika Mashariki. 

Alitolea mfano takwimu za mwaka 2024 ambapo tani 796.2 za mizigo zilisafirishwa kwa njia ya ndege kupitia Mwanza, jambo linalodhihirisha uwezo mkubwa uliopo wa kukuza usafirishaji wa bidhaa za kibiashara, huku akiwataka wafanyabiashara wanaoshiriki maonesho hayo kutumia fursa hiyo kikamilifu kutafuta wanunuzi wakubwa, wawekezaji, washirika wa kimkakati na masoko mapya badala ya kujizuia katika kuonesha bidhaa pekee.

Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF 2026) yamezinduliwa rasmi, Septemba 3, 2026, jijini Mwanza na Mhe. Dennis Londo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, yakihusisha washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo wafanyabiashara kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Zimbabwe, China, India na Singapore.

Akizungumza wakati wa ufunguzi hup Londo amesema MEATF ni jukwaa muhimu linalowaunganisha wafanyabiashara na masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), pamoja na masoko mengine ya kikanda na kimataifa.

Mhe. Londo amewataka wafanyabiashara kubadili mtazamo kuhusu ushiriki wao katika maonesho hayo, akisisitiza kuwa ushiriki haupaswi kuishia katika kuonesha na kuuza bidhaa pekee, bali utumike kama fursa ya kujenga masoko endelevu, kuanzisha mahusiano ya kibiashara na kusaini mikataba ya biashara.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wazalishaji kuendelea kuboresha bidhaa zao kwa kuongeza thamani ili ziweze kukidhi viwango na ushindani katika masoko ya nje ya nchi.

No comments