BONDIA ATUHUMIWA KUUA MWANAMKE NA KUMTIA KATIKA SANDUKU


Polisi nchini Greece wamemkamata bondia na mkimbizi kutoka Afghanistan, Sharif Ahmadzai, mwenye umri wa miaka 26, kuhusiana na kifo cha mfanyakazi wa kujitolea wa Scotland, Elisabeth Jane Ross (anayejulikana kama Lisa) mwenye umri wa miaka 38. Mwili wa marehemu uligundulika ukiwa ndani ya sanduku katika jengo lililoachwa wazi katika eneo la Kypseli mjini Athens tarehe 18 Julai, siku kadhaa baada ya kuripotiwa kupotea.

Uchunguzi wa awali wa kitabibu ulionyesha kuwa kifo hicho kilikuwa ni kitendo cha wazi cha kihalifu, huku uchunguzi wa kina ukihitimisha kuwa huenda chanzo kikaawa ni kunyongwa au kukosa hewa (asphyxiation). 

Polisi nchini Ugiriki wanachunguza uwezekano wa wawili hao kufahamiana kupitia shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ya kusaidia wakimbizi ambapo wote walikuwa wakijihusisha nayo, na inadaiwa kuwa mtuhumiwa alitumia kadi za benki za marehemu kutoa fedha.



Mshukiwa huyo, ambaye aliwasili Ugiriki akiwa kijana mdogo baada ya kupoteza wazazi wake na ndugu zake katika matukio ya kigaidi na vita nchini Afghanistan, anaishi nchini humo na mke wake wa Kimarekani na mtoto wao, ambapo waliwahi kuanzisha shirika la kusaidia wakimbizi linaloitwa Love Every Nation Athens. 

Polisi na vyombo vya ulinzi vimefanikiwa kupata ushahidi kupitia kamera za usalama (CCTV) na programu za simu zinazofuatilia mienendo ya watu (location sharing apps), zilizomwonesha mshukiwa akiwa eneo la tukio na hata akisafirisha sanduku lililokuwa na mwili wa marehemu.

Hata hivyo, wakati Ahmadzai akitarajiwa kufika mahakamani mjini Athens kukabiliwa na mashtaka yanayojumuisha mauaji ya kukusudia, unyang'anyi na makosa ya silaha, ripoti zinaeleza kuwa amekana kuhusika na mauaji hayo ingawa amekiri kuhusika na usafirishaji wa mwili huo.

No comments