URITHI WA JAHAZI WAPATA MASKANI: MAKUMBUSHO YA KWANZA YA MUZIKI YAFUNGULIWA ZANZIBAR

Waziri wa Habari, Sanaa,Utamaduni na Michezo Mh. Riziki Pembe Juma akihutubia wasanii na wadau mbalimbali wa sanaa wakati wa ufunguzi wa makumbusho ya kwanza ya muziki na nyaraka Zanzibar.



Na Beda Msimbe, BSKY Media


WAKAZI wa Zanzibar wameshuhudia kurasa mpya ya kihistoria baada ya Makumbusho ya Elimu ya Muziki na Uhifadhi wa Nyaraka za Utamaduni kufunguliwa rasmi Mji Mkongwe, Unguja. 

Tukio hilo la kihistoria lililofanyika hivi karibuni, lilitanguliwa na maandamano makubwa ya wasanii na wanafunzi waliotawala barabara kwa miondoko ya ngoma za kienyeji na beni, wakipeleka ujumbe wa amani na upendo kabla ya utepe wa ufunguzi kukatwa. 

Hazina hiyo sasa inakuwa maskani rasmi ya kuhifadhi nyimbo, vyombo vya muziki, picha, na historia za magwiji wa taarab asilia, kidumbaki, ngoma, na beni kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Muziki cha Nchi za Jahazi (DCMA), Halda Alkanaan alieleza kuwa makumbusho hayo ni ya kwanza ya aina yake Zanzibar na yatatumika kama kitovu cha elimu na utafiti kwa wageni wa ndani na nje ya nchi. 





Ndani ya makumbusho hayo, mifumo ya kisasa ya sauti inawawezesha wageni kusikiliza sauti halisi za kale za magwiji kama Siti binti Saad, huku kuta zikiwa zimepambwa na picha adimu pamoja na vyombo vya asili kama ganun, oud, na violini vinavyothibitisha mwingiliano wa kitamaduni kati ya Zanzibar na ulimwengu.

Ufunguzi huo ulienda sambamba na pongezi kwa wadau waliofanikisha ndoto hiyo ikiwemo Creation Africa kupitia Ubalozi wa Ufaransa, Alliance Francaise, UNESCO Tanzania, Sanze, na Bodi ya DCMA chini ya Mwenyekiti Bi. Salma Adim. 

Pongezi za kipekee zilimwendea mtaalamu Khamis Mohamed Kizoro, pamoja na John Kagaruki na Mohamed Muombwa kwa kujitolea kubuni na kupanga makumbusho hayo bila kukata tamaa licha ya changamoto mbalimbali za kiuendeshaji.

Hata hivyo, hafla hiyo ilitumika pia kama jukwaa la kuwasilisha changamoto zinazokabili chuo hicho, ambapo Mkuu wa Chuo, Halda Alkanaan alieleza athari za chuo kufanya kazi katika majengo ya kupanga na kuhamahama na kuiomba serikali kukipatia chuo jengo na eneo la kudumu la kulelea vipaji. 

Naye  Mwenyekiti wa Bodi, Salma Adim alitoa wito kwa jamii na wasanii kushirikiana kuendeleza makumbusho hayo kwani taifa lisilohifadhi utamaduni wake hupoteza dira na historia yake.

No comments