Sensa ya Wanyamapori: Tanzania Yaandika Historia, Yapasua Anga Kidunia




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea Taarifa ya Sensa ya Wanyamapori ya Taifa ya Mwaka 2024/2025, iliyowasilishwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) mkoani Dar es Salaam. 

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa hiyo muhimu, Mkuu wa Nchi amebainisha kuwa matokeo hayo yanaonesha mafanikio makubwa sana ya juhudi za makusudi za uhifadhi nchini, huku yakithibitisha kwa vitendo kuwa Tanzania inaendelea kushikilia nafasi ya kipekee miongoni mwa mataifa yenye utajiri mkubwa wa wanyamapori duniani. 

Rais Dkt. Samia aliipongeza kwa dhati Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na TAWIRI kwa kufanikisha zoezi hilo kubwa la kimkakati ambalo limeandika historia mpya nchini kwa kufadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali kuu kwa kutumia rasilimali za ndani.

Katika kuongeza nguvu kwenye sekta hiyo, Rais Samia ametoa maagizo mazito akitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza juhudi za makusudi katika utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda rasilimali hizo za asili. 

Lengo kuu la maagizo hayo ni kuhakikisha Watanzania wote wanaona na kuthamini urithi huo mkubwa wa taifa, na hivyo kushiriki kikamilifu katika kuutunza kwa maslahi mapana ya vizazi vya sasa na vile vijavyo.

Pia, kiongozi mkuu wa nchi amesisitiza umuhimu wa kipekee wa kuwajengea watoto na vijana wadogo uelewa wa kina wa wanyamapori wa Tanzania, hasa kwa kuwafundisha majina yao halisi ya Kiswahili ili kuimarisha utamaduni wa uzalendo na kuthamini mali asili za nchi tangu wakiwa katika umri mdogo.




Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, ametoa shukrani za dhati kwa Rais Samia kwa uthubutu na maono yake yaliyofanikisha kutengwa kwa fedha za ndani zilizowesha nchi kujitegemea na kukamilisha sensa hiyo bila kutegemea wafadhili wa nje. 

Dkt. Kijaji ameeleza kuwa sensa hii ya kitaifa ambayo hufanyika mara moja kila baada ya miaka 10, ina umuhimu mkubwa wa kibayolojia kwani inalenga kubaini idadi kamili, mtawanyiko wa kijiografia, mwenendo wa maisha, pamoja na hali ya ustawi wa wanyamapori hao huku ikasaidia kubaini changamoto zinazoweza kuathiri mifumo ya ikolojia na sekta mama ya utalii nchini.

Zoezi hilo kubwa la ukusanyaji wa takwimu ambalo lilitekelezwa kwa umakini wa hali ya juu kati ya mwezi Septemba 2024 na Oktoba 2025, limeonesha uwepo thabiti wa spishi 28 za wanyamapori wa jamii ya kati na wakubwa katika mifumo mbalimbali ya ikolojia nchini. 

Kwa ujumla, matokeo hayo ya kisayansi yanaonesha mwenendo chanya wa uhifadhi katika kipindi chote cha miaka 10 iliyopita, jambo linalothibitisha ufanisi wa doria na usimamizi wa hifadhi zetu. 

Wakati umma ukiendelea kusubiri tathmini ya kina, Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kutangaza rasmi matokeo yote ya kina na takwimu zilizokusanywa hivi karibuni kupitia kwa Waziri mwenye dhamana.

No comments