Samia Atuma Ujumbe Mzito Chato Maziko ya Mama yake na Hayati Magufuli



Makamu wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amefunguka kwa kina na kuonesha ukaribu mkubwa uliokuwepo kati yake na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Pombe Magufuli, wakati wa ibada ya mazishi ya mama mzazi wa kiongozi huyo, Bi. Suzana Ngollo, wilayani Chato mkoani Geita. 

Katika hafla hiyo ambapo alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, Dk. Nchimbi alisisimua waliohudhuria kwa kueleza namna walivyokuwa wakibishana kwa hoja na jinsi alivyomshauri asifanye siasa, ushauri uliomfanya Dk. Magufuli amteue kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil mwaka mmoja baadaye. 

Katika kuonesha ukaribu huo wa kipekee, Makamu wa Rais alichukua fursa hiyo kuwasomea wananchi ujumbe muhimu wa siri na wa kihistoria aliouhifadhi kutoka kwa hayati Dk. Magufuli.

Akiwasilisha salamu za Rais Samia Suluhu Hassan, Dk. Nchimbi ametoa mwito mzito kwa Watanzania wote kumuenzi Bi. Suzana Ngollo kama alama na kielelezo cha malezi bora ya watoto yanayotanguliza maadili mema na maslahi ya taifa mbele. Rais Samia amewasihi wazazi nchini kuwapenda na kuwaandaa watoto wao ili waweze kutumikia nafasi yoyote watakayoipata maishani. 













Dk. Nchimbi alibainisha kuwa msiba huo wa Bi. Suzana, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89 baada ya kuugua kwa muda mrefu, umekutanisha mamilioni ya watu si kwa sababu ya umaarufu wake binafsi, bali kwa sababu alizaa na kulea mtoto aliyeacha alama isiyomfutika katika utumishi wa nchi ya Tanzania.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, amesisitiza kuwa serikali mkoani humo imejizatiti kwa dhati kuyaenzi matendo mema yote yaliyofanywa na marehemu Bi. Suzana pamoja na mwanawe, Hayati Dk. Magufuli, aliyeongoza nchi kati ya mwaka 2015 na 2021. 

Katika ibada hiyo ya Misa Takatifu, Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassalla, alimtaja marehemu kama nembo ya maisha ya kiimani yaliyosimama imara ndani ya familia. Akisoma wasifu wa marehemu kwa niaba ya familia, Michael Magufuli alieleza kuwa Bi. Suzana alizaliwa Juni Mosi, 1936, na ameacha mnyororo mkubwa wa uzao unaojumuisha watoto 15, wajukuu 77, vitukuu 125, pamoja na kilembwe mmoja.


No comments