RAIS MSTAAFU KIKWETE ASHIRIKI MAZISHI YA KITAIFA YA RAIS MSTAAFU MOGAE WA BOTSWANA, AKIMWAKILISHA MHESHIMIWA RAIS SAMIA




Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, leo tarehe 16 Mei 2026 amemwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Mazishi ya Kitaifa ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa Botswana, Hayati Festus Gontebanye Mogae, yaliyofanyika jijini Gaborone. 

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Samia, Dkt. Kikwete amesema Tanzania inaungana kwa dhati na Serikali pamoja na wananchi wa Botswana katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo kufuatia kifo cha kiongozi huyo mashuhuri na mwenye ushawishi mkubwa barani Afrika.

Katika hotuba yake kwa waombolezaji, Dkt. Kikwete amebainisha kuwa wakati wa uongozi wa Hayati Mogae, ushirikiano na uhusiano wa kindugu kati ya Tanzania na Botswana uliendelea kuimarika kwa kiwango kikubwa, huku akisisitiza kuwa kiongozi huyo alikuwa rafiki wa kweli wa Tanzania na aliipenda nchi hiyo kwa dhati. 



Aidha, alieleza kuwa Hayati Rais Mogae alikuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha umoja, mshikamano na amani barani Afrika, sambamba na kushiriki kikamilifu katika juhudi mbalimbali za usuluhishi wa migogoro katika mataifa tofauti ya bara hili.

Akizungumzia uhusiano wake binafsi na Hayati Mogae, Dkt. Kikwete amesema alipata heshima ya kufanya kazi naye kwa mara ya kwanza wakati kiongozi huyo akiwa Makamu wa Rais wa Botswana, huku yeye akihudumu kama Naibu Waziri na baadaye Waziri kamili wa wizara mbalimbali ikiwemo ya Fedha chini ya Serikali za Rais Ali Hassan Mwinyi na Rais Benjamin Mkapa ambapo walishirikiana vyema ndani ya SADC. 





Ushirikiano huo uliendelea hata walipokuwa Wakuu wa Nchi zao kwa pamoja, ambapo Dkt. Kikwete amemuelezea Rais Mogae kama mtu mzuri, mwenye misimamo, mwadilifu, na ambaye siku zote alitetea kile alichokiamini kwa upole na heshima kubwa. 

Mazishi hayo ya Kitaifa yalihudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa sasa, viongozi wastaafu, pamoja na wajumbe mbalimbali kutoka ndani na nje ya Afrika waliokuja kutoa heshima zao za mwisho.


No comments