MAMA MZAZI WA MAREHEMU RAIS MAGUFULI APUMZIKA, KUZIKWA IJUMAA CHATO
Mama mzazi wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, marehemu Dk John Pombe Magufuli, Bibi Suzana Magufuli mwenye umri wa miaka 94, anatarajiwa kuzikwa Ijumaa ya tarehe 29 Mei katika makaburi ya familia yaliyopo Chato.
Suzana aliaga dunia akiwa nyumbani kwake wilayani Chato mkoani Geita kutokana na changamoto za kiafya ambazo amekuwa nazo kwa muda mrefu.
Msemaji wa familia ya Magufuli kwenye msiba huo ambaye pia ni mtoto wa marehemu, Gorodian Magufuli, alieleza waandishi wa habari kuwa uamuzi huo wa siku ya mazishi umefikiwa baada ya kikao cha familia, na mazishi hayo yatatanguliwa na ibada maalumu itakayofanyika katika Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi Mlimani Chato, Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara.
Gorodian alifafanua kuwa mama yao mzazi alianza kupata changamoto hizo za kiafya tangu mwaka 2018, ambapo alitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa miezi minne kabla ya kurejea nyumbani, na baada ya hapo amekuwa akipatiwa huduma na uangalizi wa karibu wa kimatibabu kutoka kwa madaktari bingwa wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Aliongeza kuwa mnamo tarehe 25 Mei, 2026 majira ya saa nne asubuhi, waliona hali yake imebadilika ghafla na ndipo walipompeleka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kwa ajili ya matibabu zaidi, lakini majira ya saa moja usiku wa siku hiyo alifariki dunia.
Kufuatia msiba huo mzito, viongozi mbalimbali wamejitokeza kufariji familia ambapo Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, alisema serikali itasimamia kwa ukamilifu ratiba na taratibu zote za msiba huo mpaka siku ya mwisho ya mazishi kwa kufuata maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia ametoa salamu za pole akieleza kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba huo na kuungana na familia katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, akiwaombea nguvu, faraja na uvumilivu kwa niaba yake binafsi na kwa niaba ya serikali.
Salamu kama hizo zilitolewa pia na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, aliyesema msiba huo si wa familia pekee bali ni wa Watanzania wote walioguswa na mchango mkubwa wa familia hiyo kwa taifa, huku Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, naye akituma salamu zake za rambirambi.
Taarifa za kifo cha Mama Suzana zilitolewa mwanzoni na mjukuu wake, Jesca Magufuli, kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ambapo aliandika kuwa pengo la bibi yao halitazibika kamwe lakini wanamshukuru Mungu kwa miaka yote aliyowajalia kuwa naye na kwa kazi kubwa ya malezi aliyoifanya kwao.
Wakati huohuo, Chama Cha Mapinduzi mkoani Geita kimeahidi kushiriki kikamilifu katika msiba huo ambapo Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Nicolous Kasendamila, alisema chama na serikali kwa ujumla wamepoteza mama, mzazi, na muhimili mkubwa sana katika historia ya taifa la Tanzania.
Post a Comment