SERIKALI INAVYOJIVUNIA KUTANUKA KWA ATCL




Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limeendelea kupata mafanikio makubwa kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano. 

Hadi kufikia sasa, shirika limefanikiwa kuwa na jumla ya ndege 16 baada ya kuwasili kwa Boeing 787-8 Dreamliner mwezi Agosti 2024. Ndege hizi zinajumuisha ndege za masafa marefu, kati, mafupi, na ndege moja ya mizigo.

Ukuaji wa idadi ya ndege umeiwezesha ATCL kupanua mtandao wake wa safari kutoka vituo 23 mwaka 2020/21 hadi vituo 33 mwaka 2025/26. Safari mpya za kimataifa zimezinduliwa kuelekea Lagos, Kinshasa, Accra, na miji mingine mikubwa barani Afrika. Hii imesaidia kuunganisha Tanzania na masoko makuu ya kikanda na kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akielezea mafanikio ya siku 100 za Rais Samia Suluhusu Haasan  akizungumza na waandishi wa habari katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha  Julius Nyerere(JNIA) Februari 26,2026

Katika upande wa abiria, ATCL imeshuhudia ongezeko kubwa kutoka abiria 822,232 mwaka 2021/22 hadi milioni 1.17 mwaka 2024/25. Takwimu za nusu mwaka ya 2025 zinaonyesha tayari abiria zaidi ya 700,000 wamesafirishwa. Mafanikio haya yameongeza mapato ya shirika kwa asilimia 87.88, yakifikia Dola za Marekani milioni 157.69.

Sekta ya mizigo nayo imepata mapinduzi, ambapo tani za mizigo zilizosafirishwa zimeongezeka kutoka 2,567 hadi 6,919. Ununuzi wa ndege maalum ya mizigo umerahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo na mbogamboga kwenda masoko ya nje. Hii imetoa fursa mpya kwa wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania kupata fedha za kigeni.

Serikali haina mpango wa kuishia hapo, kwani tayari mchakato wa kununua ndege nyingine nane uko katika hatua mbalimbali. Lengo ni kufikisha jumla ya ndege 28 katika kipindi kijacho ili kuimarisha zaidi utoaji wa huduma. Mipango ipo pia kuanzisha safari za Seychelles, Muscat, na Jeddah kabla ya Juni 2026.

Shirika pia limekuwa chanzo cha ajira, ambapo idadi ya watumishi imeongezeka kutoka 826 hadi 1,031. Watumishi 356 wamepatiwa mafunzo maalum katika fani za urubani na uhandisi wa ndege ili kuongeza tija. Uwekezaji huu katika rasilimali watu unalenga kuhakikisha huduma zinatolewa kwa weledi na usalama.

Kupitia kodi na tozo, ATCL imechangia shilingi bilioni 52.35 serikalini katika mwaka wa fedha 2024/25. Mafanikio haya yanathibitisha kuwa shirika linazidi kujiimarisha kibiashara na kupunguza utegemezi. ATCL sasa ni kiungo muhimu katika kukuza utalii na biashara ya kimataifa kwa Tanzania.

No comments