LUPITA NYONG’O AFUNGUKA VIMBE ZAIDI YA 50 KWENYE MJI WAKE WA MIMBA
Mwigizaji mashuhuri na mshindi wa tuzo ya Oscar Lupita Nyong’o amewashtua mashabiki wake duniani kote baada ya kufunguka kuhusu changamoto kubwa ya kiafya aliyopitia hivi karibuni ambapo aligundulika kuwa na vivimbe zaidi ya hamsini kwenye mji wa mimba maarufu kama fibroids.
Lupita alibainisha kuwa baadhi ya vivimbe hivyo vilikuwa na ukubwa unaolingana na tunda la chungwa hali iliyomsababishia maumivu makali na usumbufu uliomfanya wakati mwingine kushindwa hata kusimama au kutembea vizuri.
Katika mahojiano yake ya kina na jarida la Glamour Lupita alieleza kuwa aliamua kuweka wazi siri hiyo ili kuwapa ujasiri wanawake wengine wanaoteseka na tatizo hilo kimya kimya bila kujua wapi pa kuanzia.
Akizungumzia namna alivyokuwa akihisi mwigizaji huyo alikiri kuwa hali hiyo ilimletea msongo wa mawazo na hofu kubwa ya kihisia kutokana na jinsi mwili wake ulivyokuwa ukibadilika na kujaa mgandamizo mkubwa wa tumbo.
Alisema kuwa uvimbe huo ulimfanya ahisi kulemewa na mwili wake mwenyewe na kupoteza ujasiri wa kawaida ambao amekuwa nao wakati wa kazi zake za uigizaji. Aliongeza kuwa safari hiyo ilikuwa ya upweke mpaka alipoamua kutafuta msaada wa kitabibu na kugundua ukubwa wa tatizo lililokuwa likimkabili ndani ya mwili wake.
Kutokana na hali hiyo Lupita alilazimika kufanyiwa upasuaji wa kitaalamu uitwao Laparoscopic Myomectomy ambao unalenga kuondoa vivimbe hivyo pekee huku ukiacha mji wa mimba ukiwa salama bila madhara yoyote.
Upasuaji huo ulikuwa na mafanikio makubwa na mwigizaji huyo ameeleza kuwa kwa sasa anajihisi mwepesi na mwenye afya kama mtu aliyezaliwa upya baada ya kuondolewa kwa mzigo huo mzito. Kwa sasa Lupita yupo katika kipindi cha mapumziko na uangalizi wa madaktari ili kuhakikisha mwili wake unarejea katika hali yake ya kawaida kabla ya kurejea tena kwenye majukumu yake ya kila siku.
Lupita amesisitiza kuwa atatumia ushawishi wake kuendelea kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa fibroids akibainisha kuwa takwimu zinaonyesha wanawake weusi wana uwezekano mkubwa wa kupata tatizo hili kuliko wanawake wa rangi nyingine. Amewasihi wanawake kote duniani kutopuuza dalili kama maumivu makali ya hedhi au kuvimba kwa tumbo kusiko kwa kawaida na badala yake wafanye uchunguzi wa mapema ili kuokoa maisha yao.

Post a Comment