MASAUNI: VIJANA KUWENI WALINZI EPUKENI SUMU YA UDINI NA UKABILA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ametoa wito kwa vijana nchini kuwa walinzi wa amani na mshikamano.
Aidha amewataka kuuenzi Muungano wa Tanzania kwa vitendo ili kuulinda dhidi ya migawanyiko.
Akizungumza katika kongamano la elimu ya Muungano lililowakutanisha wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu Zanzibar, lililofanyika Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, Waziri Masauni amesema vijana wana jukumu la msingi la kuhakikisha tunu za Muungano zinadumishwa.
Amesisitiza kuwa Muungano umekuwa nguzo ya amani na utulivu kwa pande zote mbili, hivyo vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuutetea dhidi ya upotoshaji.
Waziri Masauni amewahimiza wanafunzi hao kujifunza historia ya nchi na kuelewa misingi ya umoja wa kitaifa ili kushiriki kikamilifu katika mijadala inayojenga nchi.
Kongamano hilo ni sehemu ya mikakati ya Serikali kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu umuhimu wa Muungano na nafasi ya vijana katika kuuenzi urithi huo.
Baadhi ya wananchi na wadau wameunga mkono kauli hiyo wakionya dhidi ya chuki za kidini na kikabila. Frank Joseph, mkazi wa Magole, Ilala, amesema Watanzania wanapaswa kuepuka sumu ya udini ambayo imeyatesa mataifa mengine, akisisitiza kuwa amani haina tiba ikishavurugika.
Naye Athumani Mkwizu, mkazi wa Mwanga mkoani Kilimanjaro, amewataka Watanzania kukataa kutumiwa kuiharibu nchi ambayo imejengwa kwa zaidi ya miaka 60 tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Amesema ni aibu kwa kizazi cha sasa kubomoa mshikamano uliodumu kwa miongo mingi.
Kwa upande wake, Saidi Gulu, mjasiriamali kutoka Temeke, amesema amani ndiyo msingi wa ustawi na maendeleo ya Taifa, akibainisha kuwa ushindani wa kisiasa unapaswa kujikita katika sera na ajenda za maendeleo badala ya mivutano inayoweza kuhatarisha umoja wa nchi.

Post a Comment