RC MBONI MHITA AWAFUNDA VIJANA NIDHAMU YA UWAJIBIKAJI NA KUSAKA FURSA
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Mboni Mhita, amewataka vijana nchini Tanzania kuzingatia nidhamu ya uwajibikaji na kuwa na uthubutu wa kusaka fursa ili kufikia malengo yao katika maisha na uongozi.
Akizungumza katika mkutano wa vijana wa Fikrah Summit hivi karibuni, Mhe. Mhita alieleza kuwa anaona fahari kuendelea kuwainua wadogo zake kwa kuwashirikisha uhalisia wa safari yake ya maisha ya uongozi.
Alisisitiza kuwa siri ya mafanikio kwa kiongozi yeyote, hususan kwa wasichana, inatokana na kujituma kwa dhati na kufanya maamuzi ya kutoishia kwenye kushindwa bali kusimama imara kufuata hatua za mafanikio zilizowekwa na waliotangulia.
Katika mazungumzo yake na vijana hao, kiongozi huyo alibainisha kuwa kila msichana anazaliwa na uwezo wa uongozi ndani yake, hivyo kinachotajika ni nidhamu na uwezo wa kuthubutu kupambana na hali iliyopo bila kukata tamaa. Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele kikubwa katika kuhakikisha ustawi wa jamii na kutoa mazingira wezesha kwa vijana kujikwamua kiuchumi na kijamii kupitia fursa mbalimbali.
Mhe. Mhita alitumia wasaa huo kubadilishana mawazo na kusikiliza maoni ya vijana hao ambapo aliwakumbusha kuwa safari ya maisha ya uongozi inahitaji unyenyekevu na uwezo wa kubeba majukumu kwa neema, huku mtu akijivunia mafanikio na kujifunza kupitia changamoto zinazojitokeza. Alimalizia kwa kuwatakia vijana hao mafanikio mema na kuahidi kuwa ataendelea kuwa mstari wa mbele kuhamasisha na kutoa dira kwa kizazi kipya ili kiweze kuingia kwenye nyanja za uongozi na uwajibikaji kikiwa kimeiva na tayari kulitumikia taifa.
Ujumbe wake umepokelewa kwa hamasa kubwa na wadau mbalimbali ambao wamemuelezea kama kiongozi mjasiri, muungwana na mfano wa kuigwa anayejua namna ya kutoa hamasa bila kuathiri misingi ya kazi. Wengi wamemtaja kama kiongozi anayemiliki vyema majukumu yake na kutoa funzo kwa wasichana wengi nchini Tanzania kuwa na uthubutu wa kuandika historia zao kwa kutumia uwezo waliojaliwa na Mungu katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii zao.

Post a Comment