MCHUJO WA MADEREVA WA PIKIPIKI 500 KWENDA DUBAI KUFANYIKA NCHI NZIMA
Katika kuelekea kutimiza malengo ya Dira ya Maendeleo ya 2050, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira ya utulivu kwa vijana nchini kwa kufungua milango ya ajira nje ya nchi.
Kutokana na kuwapo kwa milango hiyo wazi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, Januari 8,2026 amewaaga vijana 109 ambao wamepata kazi ughaibuni kupitia mawakala takribani 15 wanaofanya kazi kwa karibu na serikali. Aidha alisema kuna jumla ya ajira 70,000 zinasubiri ukamilishwaji.
Hafla hiyo ya kuaga imeambatana na mapokezi ya vijana wengine 94 ambao wamerejea nchini baada ya kukamilisha mikataba yao ya kazi kwa ufanisi mkubwa nchi za nje.
Waziri Sangu ameeleza kuwa serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha Watanzania wanapata kazi zenye staha zinazozingatia sheria za kimataifa za kazi hasa za Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO).
Kundi hili linaloondoka linajumuisha kada mbalimbali wakiwemo mafundi mchundo, wajenzi, mafundi umeme, waendeshaji mitambo, wahudumu wa maabara, wauguzi na wahudumu wa ndani. Hii ni sehemu ya juhudi kubwa ambapo tangu Novemba mwaka jana hadi sasa, watu 1,432 wamefanikiwa kupata kazi katika nchi kama Ujerumani, Denmark, Bahrain, Falme za Kiarabu na Kuwait.
Ili kuongeza wigo wa ajira na kuleta uchumi shindani, Waziri amewaagiza maafisa wa ajira kuhakikisha mchujo wa madereva wa pikipiki 500 wanaohitajika Dubai unafanyika nchi nzima ili kila kijana mwenye sifa apate fursa. Aidha, amebainisha uwepo wa fursa nyingine 8,000 zinazofanyiwa kazi, ikiwemo nafasi 10,000 za uuguzi nchini Saudi Arabia, na nafasi nyingine kama hizo Kuwait na Falme za Kiarabu.
Serikali imesisitiza kuwa kwa sasa, kutokana na diplomasia ya uchumi ya Rais Samia, Tanzania imevuka hatua ya kutoa nguvu kazi isiyo na ujuzi na sasa inatoa wataalamu (professionals) katika soko la nje.
Kuwezesha vijana kwenda nje kunasaidia kupunguza shinikizo la ajira nchini na kuongeza mzunguko wa fedha za kigeni pale vijana hawa wanapotuma fedha nyumbani, jambo ambalo ni muhimu katika kujenga uchumi imara na shindani duniani.

Post a Comment