SADC NA PENGO LA MAWASILIANO YA SAYANSI



Pretoria, Afrika Kusini

Wakati ulimwengu ukiwa katika kasi ya ajabu ya kiteknolojia, kukiwa na ubunifu kama Akili Bandia (AI) na roketi kuvuka anga, imebainika kuwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) bado zinakabiliwa na pengo kubwa la mawasiliano ya sayansi kwa umma.

Hali hii inasababisha matokeo ya utafiti na ugunduzi mbalimbali wa taasisi za kisayansi 'kutotembea' kwa kasi, na kushindwa kuwafikia wananchi vema ili kujenga uelewa wa sayansi kama sehemu ya maisha ya kila siku.



Mkazo wa SADC Kukosa Mikakati

Haya yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa na Afrika, Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (DSTI), Afrika Kusini, Mwampei Chaba, wakati akifungua mdahalo wa siku moja wa waandishi wa habari za sayansi kutoka nchi 18 wanachama wa SADC.

Mdahalo huo umefanyika jijini Pretoria sambamba na Mkutano wa Kimataifa wa Waandishi wa Habari za Sayansi (WCSJ2025).

Bi. Chaba aliweka wazi chanzo cha pengo hilo akisema:"Nchi nyingi katika SADC bado hazina mkakati wa ushirikiano katika mawasiliano kuhusu sayansi. Hiyo ndiyo sababu upashanaji habari za sayansi unakumbwa na changamoto nyingi.”

Alisema ukosefu wa mkakati huo unawafanya waandishi wa habari kukosa ushirikiano kutoka serikalini, kukosa fursa za ufadhili, na kushindwa kuwa karibu na watafiti.


Wito kwa Waandishi Kufuatilia

Bi. Chaba amewahimiza waandishi kurudi nyumbani na kuuliza wizara zinazohusika na sayansi na mawasiliano iwapo zimeandaa mkakati wa mawasiliano ya sayansi.

Alisisitiza kuwa Serikali za SADC hazitaweka kipaumbele cha kutosha na kuongeza ufadhili wa sayansi ikiwa thamani na athari zake hazijulikani kwa jamii na serikali.

“Ninyi ndio midomo yetu. Ninyi ndio mabalozi wetu wa kuwasilisha sayansi kwa jamii,” alisema. “Jukumu lenu ni muhimu sana, na tunategemea ninyi kusaidia kuunganisha pengo.”



Kujenga Uwezo na Historia Mpya

Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo, Bi. Chaba alieleza kuwa DSTI iliona vema kuwaunganisha waandishi wa SADC kwa lengo la kujenga uwezo wao katika uandishi wa sayansi.

“Pia tuligundua kuwa waandishi wa sayansi bado hawana uwezo wa kutosha kuhusiana na uandishi na kuandika makala za sayansi,” alibainisha.

Aidha, alibainisha kuwa huu ni mkutano wa kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa Bara la Afrika kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa waandishi wa habari za sayansi.



Fursa ya Majukwaa ya Kidijitali

Katika kuhakikisha sayansi inafikia jamii pana, Bi. Chaba alihimiza matumizi bora ya majukwaa ya kidigitali, hasa kwa kundi la vijana.

“Kila mtu yupo TikTok, kila mtu yupo YouTube, lakini lazima tuone maudhui ya sayansi pia kwenye TikTok au YouTube… Tumia majukwaa haya maarufu kuwasilisha sayansi,” alisisitiza.

Alifunga kwa kutoa changamoto kwa waandishi waliohudhuria: “Afrika inahitaji sayansi kwa maendeleo zaidi kuliko kanda nyingine yoyote duniani. Tufanye lengo letu kuwa na waandishi mashuhuri wa sayansi katika jamii zetu, nchi zetu, ndani ya SADC na barani kote.”

No comments