WAINGEREZA WAJIHOJI UHABA WA WASHAMBULIAJI WA KATI



WAINGEREZA wapo katikia shaka kubwa huku wakijiuliza kulikoni kumekuwa na kupungua kwa washambuliaji wa kati yaani 'Namba Tisa' wakali, wanajiihoji bomba hizo zimepotealea wapi.

Wachambuzi wa soka wa Uingereza wanakiri kwamba  amebaki mmoja tu.

Ukweli huo umebainika baada ya  kocha Thomas Tuchel kutangazwa kwa kikosi chake hivi karibuni. Kikosi hicho kimefichua uhaba mkubwa wa washambuliaji wa kati (centre-forwards) Waingereza, huku Harry Kane akiwa ndiye mshambuliaji pekee kamili (out-and-out striker) katika kundi la wachezaji 25 waliochaguliwa.

Inakubalika kuwa hili linachangiwa kwa kiasi na majeraha; Tuchel alieleza kuwa Ollie Watkins amepumzishwa ili kudhibiti tatizo linalomsumbua, huku Dominic Solanke akiwa nje ya uwanja tangu Agosti, na Liam Delap ameanza kurejea Chelsea baada ya kukaa nje miezi miwili.

Ingawa wapo washambuliaji wengine wenye uwezo wa kucheza nafasi tofauti wamechaguliwa kama Marcus Rashford, Jarrod Bowen, Phil Foden, na Anthony Gordon huenda hao si ‘Namba Tisa’ wa kimila, lakini wanaweza kuombwa kucheza katikati katika mechi dhidi ya Serbia na Albania wiki hii.

Licha ya hayo, kuona jina la Kane pekee kama mshambuliaji wa kweli ni ukumbusho mkali wa jinsi Uingereza inavyomtegemea mno mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 kama nguzo kuu ya mashambulizi yao. Uhaba wa chaguo jingine la kuongoza safu ya ushambuliaji ni wasiwasi mkubwa kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia msimu ujao wa joto, na hata hapo baada ya hapo.

Kane amekuwa na ufanisi mkubwa katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) akiwa na Bayern Munich msimu huu. Hata hivyo, ni washambuliaji wanane tu Waingereza walioonekana kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League) katika kampeni inayoendelea, na Delap, mwenye umri wa miaka 22, ndiye pekee aliye chini ya umri wa miaka 26.



Nyuma ya Delap, hakuna kizazi kipya 


Timu ya Taifa ya Uingereza ya Vijana Chini ya Miaka 21 ilikwenda kwenye Mashindano ya Uropa msimu uliopita wa joto bila mshambuliaji anayetambulika. Kikosi chao cha hivi karibuni kinajumuisha mshambuliaji mmoja tu, Divin Mubama wa Manchester City (21), ambaye bado hajafunga bao lolote katika Premier League na kwa sasa yuko kwa mkopo katika timu ya Stoke inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (Championship).

Kwa hivyo, wamepotelea wapi ‘Namba Tisa’ wote Waingereza, na kwa nini nchi hii haizalishi tena washambuliaji wa kiasili?

Wachambuzi wanasema kuna baadhi ya washambuliaji Waingereza wapo huko nje, lakini ukiangalia takwimu zao, si za kutia moyo sana.

Danny Welbeck, ambaye anatimiza miaka 35 mwishoni mwa mwezi huu, na Callum Wilson, mwenye miaka 33, ndio pekee waliofunga zaidi ya bao moja katika Premier League msimu huu.

Miongoni mwa wale wanaozingatiwa na Tuchel wanaocheza mbali na ligi, Ivan Toney ndiye mwenye ufanisi zaidi katika kampeni inayoendelea, akiwa na mabao 11 katika mechi 15 akiwa na klabu ya Al-Ahli ya Ligi Kuu ya Saudi Arabia, aliyojiunga nayo mwaka 2024.

Tuchel alimchagua mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 kwa ajili ya mechi dhidi ya Andorra na Senegal mwezi Juni, lakini Toney alicheza kama mbadala (substitute) tu kwa dakika ya 88 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Senegal, na hajachaguliwa katika kikosi kingine chochote tangu wakati huo.

Kutokana na ukweli huo wachambuzi wanasema kwamba uhaba huu wa 'Namba Tisa' hautokani na kushuka ghafla kwa idadi. Badala yake, ni changamoto ambayo imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu.Msimu uliopita, washambuliaji watatu tu Waingereza – Watkins (16), Delap (12) na Welbeck (10) – walifunga mabao 10 au zaidi ya Premier League. Hii ndiyo idadi ndogo zaidi kuwahi kutokea.

Hali hii inatofautiana sana na msimu wa kwanza wa enzi ya Premier League (1992-93), ambapo washambuliaji 20 Waingereza walipitisha alama ya mabao 10.Katika miaka ya hivi karibuni, hata hivyo, kile ambacho tayari kilikuwa kinashuka kimeanguka zaidi. Msimu uliopita, mabao 67 tu yalifungwa na washambuliaji Waingereza, chini ya nusu ya idadi ya mabao katika msimu wa 2020-21.

Kuondoka kwa Kane kutoka Tottenham kwenda Ujerumani kulichangia, bila shaka, lakini aliondoka kwenda Bayern mwaka 2023 na bado washambuliaji Waingereza walifunga mabao 96 katika msimu wa 2023-24.

Hadi sasa, washambuliaji Waingereza wamefunga mabao 11 tu kwa ujumla, na wanaelekea kwenye jumla ndogo ya mabao 38 tu, ikiwa wataendelea kwa kasi yao ya sasa.

Hayo ni mabao manne tu zaidi ya yale ambayo Andy Cole na Alan Shearer kila mmoja alifunga walipoongoza chati za wafungaji wa Premier League miaka 30 iliyopita.

Sababu za Kushuka

Kulingana na mchambuzi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza,BBC, Chris Sutton, kushuka kwa washambuliaji Waingereza kunatokana na sababu kadhaa. Sutton mwenyewe alivuka alama ya mabao 10 katika kampeni nne tofauti za Premier League. Sababu moja ni ukosefu wa kucheza mechi za kutosha. Katika Premier League msimu huu, ni Welbeck, Watkins, na Calvert-Lewin pekee wameanza mechi zaidi ya tatu za ligi, huku Nketiah, Solanke, na Barnes hawajaanza hata moja.

"Ukiangalia miaka ya 1990, wachezaji kama Jurgen Klinsmann na Dennis Bergkamp walianza kuwasili kutoka nje, lakini idadi ya washambuliaji wa kigeni ilikuwa chini sana," Sutton alieleza.

"Mshambuliaji namba moja wa zama zangu alikuwa Shearer, lakini ukiangalia timu, kulikuwa na washambuliaji wengi Waingereza mahiri kama Ian Wright, Les Ferdinand, Andy Cole, Teddy Sheringham, Robbie Fowler, na David Hirst.

"Wote walikuwa wakicheza kila wiki, kwa sababu ni washambuliaji wangapi Waingereza wanaanza kucheza kwa vilabu vyao katika Premier League sasa? Hii inatokana na ubora ambao vilabu vinaweza kuvutia kutoka sehemu nyingine.

"Mabadiliko mengine ni jinsi timu zinavyopangwa. Sasa timu chache sana hucheza na washambuliaji wawili," Sutton aliongeza.

Je, Watu Waliacha Kutaka Kuwa Washambuliaji?

Shearer, ambaye aliunda ushirikiano hatari wa 'SAS' (Shearer And Sutton) na kuisaidia Blackburn kushinda taji la Premier League mwaka 1995, anahisi mabadiliko ya kiufundi  katika miaka 10 hadi 15 iliyopita ndio sababu kubwa ya uhaba wa sasa.

"Kwa sababu ya jinsi watoto wanavyofunzwa, hakuna anayetaka kucheza kama mshambuliaji wa kati kwa sababu ni nadra sana kugusa mpira," nahodha huyo wa zamani wa Uingereza aliiambia podikasti ya The Rest is Football.

"Badala yake, makocha wanataka pasi kutoka kwa kipa, pasi upande, kisha pasi kwenda kiungo... na kisha inarudi nyuma. Kama mshambuliaji wa kati unafikiri ‘sihusiki’."

Michael Owen, ambaye alishiriki Tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Premier League na Sutton akiwa na umri wa miaka 18 (1997-98) na kushinda tuzo hiyo peke yake mwaka uliofuata, anahisi asingezingatiwa kama mshambuliaji kamili ikiwa angeanza sasa.

"Katika mchezo wa leo, nadhani ningekuwa mmoja wa wachezaji wa pembeni," aliiambia podikasti ya Rio Ferdinand Presents. "Sidhani kama nilikuwa na umbo la kuwazuia mabeki wawili, kwa hivyo nadhani ningecheza upande wa kushoto."

'Tunaye Kane, Lakini Baada ya Hapo?'

Chris Sutton anaamini hali ni mbaya: "Tuna Kane, lakini baada ya hapo? Ikiwa wewe ni mshambuliaji wa kati Mwingereza sasa na unaweza kupiga mpira moja kwa moja, una nafasi nzuri ya kwenda Kombe la Dunia. Najisikia kupukuta viatu vyangu mwenyewe."


No comments