TANZANIA YAIDUWAZA NEW ZEALAND KATIKA FUTSAL, KOCHA APONGEZA TIMU




Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake ya Futsal, Curtis Reid, ametoa pongezi za dhati kwa wachezaji wake kufuatia ushindi wa kihistoria wa mabao 4-2 dhidi ya New Zealand uliofanyika juzi. Ushindi huo umefanya Kundi C kuwa na ushindani mkali kuelekea hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia.

Akizungumza jana, Kocha Reid alisema ameridhishwa na kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na wachezaji wake, ambao walifanya vizuri kwa kufuata kikamilifu maelekezo yote ya kiufundi.

"Najivunia sana wao (wachezaji). Wamekuwa wakicheza kwa kupambana sana. Tumecheza mechi nyingi za majaribio na faida zake tumeziona," alisema Kocha Reid.

Aliongeza kuwa ushindi huo ni jitihada kubwa za wachezaji na unatia moyo zaidi kwa sababu hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushiriki mchezo huo katika mashindano makubwa kama Kombe la Dunia.

"Futsal inatakiwa kuheshimika maana imetufanya tumecheza Kombe la Dunia. Naishukuru TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) chini ya Rais wake Wallace Karia kwa sapoti wanayotupatia," alieleza Kocha huyo.




Kinyang'anyiro cha Robo Fainali Kundi C

Ushindi huo unaifanya Tanzania kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi C, ikiwa na pointi 3 sawa na Japan iliyo nafasi ya pili. New Zealand inashika mkia bila pointi, huku Ureno ikiwa kinara kwa pointi sita baada ya kushinda mechi zake mbili.

Ureno sasa inahitaji pointi moja tu ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu robo fainali. Kwa upande wa Tanzania, inahitaji ushindi muhimu dhidi ya Japan katika mechi inayotarajiwa kuchezwa kesho ili kukata tiketi ya kihistoria ya kuingia hatua ya robo fainali.

Hadi sasa, hakuna timu yoyote iliyojihakikishia kufuzu hatua hiyo mpaka mechi za mwisho za makundi zitakapokamilika.


Siyame  na Kiatu cha Dhahabu

Katika habari njema zaidi, mchezaji wa Tanzania, Mary Siyame, yupo kwenye kinyang'anyiro cha kuwania tuzo ya Kiatu cha Dhahabu (Golden Boot) baada ya kufunga mabao matatu.

Mary anashindana na wachezaji wengine wenye mabao matatu kama Emily (Brazil), Vane Sotelo (Hispania), Ana Azevedo (Ureno), Sara Boutimah (Italia), Sara Oino (Japan) na Derika Peanpailun (Thailand). Kinyang'anyiro hicho kinaongozwa na Renata Adamatti wa Italia, ambaye amepachika mabao manne.


No comments