POLISI WAENDELEA KUMSUBIRI HUMPHREY POLEPOLE KWA MAHOJIANO
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Jeshi la Polisi nchini limethibitisha kwamba bado linaendelea kumsubiri aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi, Ndg. Humphrey Polepole, aripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kwa mahojiano.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu ya Polisi Dodoma, imeeleza kuwa Ndg. Polepole ambaye pia alishawahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo ya ubalozi alitumiwa barua ya wito kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ndg. Polepole anatakiwa kufika ofisini hapo ili "atoe maelezo kuhusu na tuhuma mbalimbali alizozitoa kupitia Mitandao ya Kijamii lakini hadi leo hajatekeleza maelekezo hayo kwa mujibu wa Sheria." ilisema sehemu ya taarifa hiyo kutoka polisi.
Jeshi la Polisi limefafanua kuwa wito huo unalenga kumpa fursa Ndg. Polepole kujibu na kutoa maelezo kwa mujibu wa sheria za nchi kuhusu tuhuma hizo.
Aidha, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa limeona taarifa zinazosambazwa kwenye Mitandao ya Kijamii, zinazodaiwa kutolewa na ndugu zake kwamba ndugu Polepole ametekwa, na kwamba tayari wameanza kufanyia kazi taarifa hizo.
"Jeshi la Polisi limeona taarifa zinazosambazwa kwenye Mitandao ya Kijamii na ndugu zake kuwa ametekwa, tayari tumeanza kufanyia kazi taarifa husika ili kupata ukweli wake," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Jeshi la Polisi limehitimisha kwa kusisitiza kuwa bado linaendelea kumsubiri Ndg. Humphrey Polepole aripoti Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.

Post a Comment