PLUMPTRE AKIRI KUUMIZA MASHABIKI KWA KUHAMIA SAUDI ARABIA



Mchezaji wa Kimataifa wa Nigeria, Ashleigh Plumptre, ambaye anatikisa ulimwengu wa soka la wanawake amesema wakati anaamua kujiunga na timu ya soka ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia aliwaumiza sana mashabiki wake hasa wa kundi la Wanawake wanaovutiwa na wanawake wenzao(LGBT). 

Beki huyo wa zamani wa Leicester City amekuwa  mchezaji wa kwanza kuhamia Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudi (SWPL) kutoka Ligi Kuu ya Wanawake ya Uingereza (WSL) mwaka 2023.

Plumptre, ambaye ni mchezaji mwenye fikra kali na mwenye vipaji, anakiri kwamba majibu yake ya awali kwa ofa ya Saudia ilikuwa "Hapana." Hata hivyo, baada ya mazungumzo marefu na ziara ya Mashariki ya Kati, aliona  ndio inamletea "ndoo ya dhahabu". 

Mwaka huu akisaini mkataba mwingine wa miaka miwili anataka kuonesha kwamba nchi za Magharibi zina dhana potofu kuhusu maisha ya mwanamichezo mwanamke huko Saudia.

Anakubali kuwa athari za kuumiza hisia za mashabiki wa LGBT zinamgusa.

Alipoulizwa kuhusu athari mbaya alizopokea kutoka kwa makundi ya mashabiki wa Leicester, alisema, “Wakati nilipohamia huku, athari ilikuwa mbaya kabisa. Ilikuwa ngumu. Ilionekana kama sikuwa tena mtu waliyemjua. Niliumiza hisia zao sana kwa sababu wanahisi ninawakilisha kitu kinachowafanya wajisikie hawana thamani, na ninaelewa hilo.”

Licha ya utata huo, Plumptre, ambaye anaishi katika eneo maalumu kama wafanyakazi wengi wa kigeni, anasema anahisi "yuko salama na mtulivu" huko Jeddah kuliko Uingereza. Anafananisha maisha hayo kama "mapovu ya amani," akitoa mfano wa kuacha gari lake likiwa na ufunguo ndani kwenye kishubaka cha ghorofa bila hofu, jambo ambalo hawezi kulifanya Uingereza.

Hata hivyo Plumptre anakiri kiwango cha soka la Huko Saudia bado hakijafikia kasi ya WSL. Anasema wachezaji wa kimataifa kama yeye na Asisat Oshoala wana mzigo mkubwa wa kuongeza ubora wa wachezaji wenyeji.

"Tatizo kubwa zaidi ni uhaba wa mashabiki katika michezo, jambo ambalo analiona linahitaji kujengwa kwa kuanzisha mipango ya jamii na kuwapa watoto fursa ya kuhudhuria" anasema.

Plumptre anamaliza kwa kupiga breki kuhusu matarajio ya Saudia kuandaa Kombe la Dunia la Wanawake. Anasema: “Katika siku za usoni ningesema ‘hapana’… Sihisi timu ya Saudia iko tayari kwa jukwaa kubwa la namna hiyo, itakuwa si haki kwao na kwa soka la wanawake.” Anataka maendeleo yawe ya "hatua za makusudi na za kupimika" ili yakue kwa kudumu.

No comments