Samia aijaza Manoti Stars

 

RAIS Samia Suluhu Hassan ameiwazadia timu ya soka ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Sh milioni 200 kuelekea mchezo wa robo fainali wa michuano ya Mabingwa wa Afrika kwa wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) dhidi ya Morocco utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kesho.

Fedha hizo zimewasilishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, alipoitembelea timu hiyo jana na kuwapongeza kwa hatua kubwa waliyofikia pamoja na kuwatakia heri kwa mchezo ujao.

“Nimekuja kambini kuwatembelea Taifa Stars ambao wako kambini kwa ajili ya mashindano ya CHAN na sababu kubwa ya kuja kuwatembelea ni kuwapongeza kwa hatua waliyofikia ya kufuzu robo fainali ya mashindano ya Chan 2024 pia kuwatia shime kwa mechi ya Ijumaa dhidi ya Morocco.

“Leo Mheshimiwa Rais Dk Samia amenituma salamu maalumu ya kuleta zawadi ya kuwapa moyo kabla ya mechi dhidi ya Morocco Sh milioni 200 ili kuwahimiza na kuwatia moyo mfanye vizuri zaidi katika mechi hiyo na hii haiondoi ahadi zingine ambazo zimekuwa zikitolewa,” alisema Profesa Kabudi

Alisema amewaona wachezaji wana ari, moyo na dhamira na kuwataka Watanzania wajiandae kwa ushindi na baada ya hapo kuendelea katika nusu fainali na hatimaye fainali.

Kadhalika alisema Rais Samia kabla ya kuanza kwa mashindano amewekeza fedha nyingi katika miundombinu na kwenye timu yenyewe na tangu mashindano yaanze amekuwa akifuatilia mechi zinavyokwenda na kama alivyokuwa amefanya ameahidi goli la mama amekuwa anakitoa kila walipofunga goli.

Pamoja na Sh milioni 200 Taifa Stars wanakwenda kwenye mechi hiyo wakiwa na Sh milioni 260 ambapo Azam wametoa Sh milioni 50 na NMB waliotoa Sh milioni 10.

No comments