KARIA : SITALIPA KISASI

 



*Aahidi bodi huru ya ligi

Na Rahel Pallangyo, Tanga

RAIS mteule wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ameahidi bodi huru ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Karia aliyethibitishwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu juzi kuendelea kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka minne, alisema TFF itabaki kutunga kanuni na Bodi ya Ligi Kuu itasimamia kanuni hizo.

Alisema ile kutaja TFF/Bodi ya Ligi wameiondoa kwenye kanuni na kubaki Bodi ya Ligi kwa sababu kelele nyingi zimetoka kwenye masuala ya uwezeshaji wa Bodi ya Ligi.

"Ile kutaja TFF/Bodi ya Ligi tumeiondoa kwenye ‘document’ (nyaraka) zote na mpaka kwenye kanuni tumeondoa, sisi tutabaki kutengeneza kanuni na wao watakuwa wanazisimamia maana kelele nyingi zimetoka kwenye masuala yale ya uwezeshaji wa Bodi ya Ligi Kuu, hivyo masuala ya bodi Karia hahusiki tena, tusitiane vidole vya macho bure," alisema Karia.

Alisema shirikisho lina mambo mengi ya kusimamia maendeleo ya mpira wa miguu kwani hata kituo cha Mnyanjani, Tanga kimekuwa FIFA Talent Academy.

Karia aliwashukuru wote waliofanikisha uchaguzi huo kumalizika kwa amani na kwamba sasa ameweka mkazo kwenye kuendeleza mpira wa miguu Tanzania.

"Nawashukuru wadau wote; jambo letu limekwisha salama, niwahakikishie Watanzania kuwa nitaendelea kusimamia mpira wa miguu.

Aidha, Karia aliahidi kushirikiana na watu wote na wala hana dhamira ya kulipa kisasi kwa sababu yote yaliyofanyika ni michakato ambayo Mungu alipanga wao wapite ili kuwa bora zaidi.

"Haikuwa rahisi kwa mchakato huu wa uchaguzi na wajumbe msiumie kwa nyakati ngumu zilizotokea hivi karibuni kwani hatua hiyo imekuwa ni sawa na kupitisha chuma kwenye moto ili kiwe imara.

"Misukosuko tuliyopitia ni ishara kwamba tuna changamoto kwa hiyo tunatakiwa kwenda kuzifanyia kazi na nawashukuru kwa imani yenu kwangu na wenzangu, kitu tunachotakiwa kufanya sasa ni kila mmoja akafanye kazi yake, tutakwenda kuendelea kusimamia uendeshaji mzuri wa mpira wetu," alisema Karia.

No comments