CECAFA KUZIPIMA TIMU ZA CHAN 2024
Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Vyama vya Soka Ukanda wa Afrika Mashariki na (CECAFA) limeandaa mashindano maalum kwa ajili ya timu zinazoshiriki fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN).
Mashindano hayo yamepewa jina la CECAFA 4 Nations Tournament yatakayoshirikisha timu nne yatafanyika kuanzia Julai 21 hadi 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Black Rhino Karatu jijini Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka CECAFA, mashindano hayo yatajumuisha mataifa ya Tanzania, Uganda, Kenya na Congo Brazzaville, kwa lengo ni kuzipa maandalizi kabla ya mashindano ya CHAN 2024 yatakayoanza Agosti 2 mwaka huu.
CECAFA imeamua kuziandaa timu za ukanda wake zinazoshiriki CHAN 2024 yatakayochezwa Tanzania, Kenya na Uganda ili kuzisaidia kupima mifumo yao, kutathmini mmunganiko wa timu na kufanya marekebisho ya mwisho.
Kikosi cha Taifa Stars kipo kambini Misri kuanzia Julai 7 mwaka huu wakijiandaa na michuano ya CHAN itashirikisha timu kutoka mataifa 19.
"Lengo kuu la mashindano haya ni kuzipa timu zetu jukwaa muhimu kujiandaa vya kutosha kabla ya Michuano ya Mataifa ya Afrika," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA Auka John Gecheo.
Mashindano hayo kila timu itacheza mechi tatu na timu itakayokuwa na nyingi baada ya mechi zote itatangazwa mshindi.
Julai 21, Harambee Stars itamenyana na Uganda Cranes, huku Tanzania ikimenyana na Congo Brazzaville.
Julai 24, Uganda itamenyana na Congo, huku Tanzania ikimenyana na Kenya.
Raundi ya mwisho inatarajiwa kutoa maarifa muhimu kuhusu utayari wa kila timu CHAN.
Kocha Mkuu wa Kenya, Benni McCarthy amefurahia mpango huo, na kuuita "mazoezi bora" kwa mashindano hayo.
"Itakuwa fursa nzuri sana kuona wachezaji wakiwa katika mpangilio wa kiushindani," alisema McCarthy.
"Hii pia ni nafasi kwetu kutathmini mifumo ambayo tumeifanyia kazi na kuona jinsi wachezaji wanavyocheza kwenye mechi za ushindani. Ni muhimu ili kuongeza kasi kabla ya mchezo wetu wa ufunguzi dhidi ya DR Congo".
Timu hizo nne zimepangwa katika makundi tofauti kwa CHAN 2024: Kenya katika Kundi A, Tanzania Kundi B, Uganda Kundi C, na Congo Brazzaville katika Kundi D.
Kenya itafungua kampeni ya CHAN Agosti 3 dhidi ya DR Congo katika Uwanja wa Moi, Kasarani, Tanzania itamenyana na Burkina Faso katika ufunguzi wa michuano hiyo Agosti 2 Dar es Salaam, wakati Uganda itacheza na Algeria Agosti 4, ikifuatiwa na pambano la Congo na Sudan Uwanja wa New Amaan Zanzibar siku inayofuata.

Post a Comment