Pages

Saturday, July 20, 2024

Timu ya Olimpiki yaagwa, yatamba

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Suleiman Serera (kushoto) akimkabidhi bendera ya taifa nahodha wa timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya Olimpiki Paris, Ufaransa, Alphonce Simbu, katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana. Kulia ni Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashind, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Henry Tandau na Katibu Mkuu  Filbert Bayi.

TIMU ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 33 ya Olimpiki Paris, Ufaransa imeagwa na kusema wako tayari kuitetea bendera ya taifa.

Akizungumza katika hafla ya kuiaga timu hiyo Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana, nahodha Alphonce Simbu alisema wamejiandaa vizuri na wako tayari kwa mapambano.

Alisema anajua Michezo ya Olimpiki ni migumu na inashirikisha nyota na magwiji wa riadha duniani ila wamejipanga kuweka historia kwa kurudi na medali.

"Huu ni mwaka wetu, maandalizi tuliyofanya hakuna shaka tutakuwepo ndani ya tatu bora, mwaka huu Tanzania itafanya vizuri,” alisema Simbu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Suleiman Serera aliwataka wachezaji hao kwenda kupambana kwani wameandaliwa vizuri.

"Rais Samia Suluhu Hassan ametutuma tuwaeleze kuwa atafuatilia mashindano yenu, nchi iko pamoja na ninyi na serikali itawagharamia posho zenu ili mwende Paris bila mawazo," alisema.

Alitaka mashirikisho na vyama vya michezo kuanza maandalizi mapema kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya 34 itakayofanyika Los Angeles, Marekani 2028.

Hata hivyo, Dk Serera amewashauri wanamichezo kujitunza akimtolea mfano Simbu ambaye alisema mwaka 2015 yeye Serera akiwa masomoni, Beijing China mwanariadha huyo alikuwa anatamba na hadi sasa bado anafanya vizuri.

Mkuu wa msafara kwenye michezo hiyo, Henry Tandau alisema safari ya timu imekamilika na kwenye ufunguzi bendera ya Tanzania itabebwa na Sophia Latiff na Andrew Mlugu.

"Nahodha (Simbu) kwenye ufunguzi atakuwa hajawasili Paris,” alisema Tandau.

Wachezaji wanaounda timu hiyo ni waogeleaji Collins Saliboko na Sophia, mcheza judo Mlugu na wanariadha, Jackline Sakilu, Magdalena Shauri, Simbu na Gabriel Geay wote wanakimbia marathoni.

Wengine katika msafara huo ni makocha, Anthony Mwingereza (riadha), Alex Mwaipasi (kuogelea) na Innocent Mallya (judo) watakaoambatana na mkuu wa msafara Henry Tandau, mwandishi wa habari Muhidin Michuzi na daktari wa timu, Eliasa Mkongo.

Tanzania hadi sasa haijawahi kutwaa medali katika Michezo ya Olimpiki tangu mwaka 1980 wakati Filbert Bayi na Suleiman Nyambui waliposhinda medali za fedha za meta 3,000 kuruka gogo na maji na meta 5,000.

No comments:

Post a Comment