Pages

Saturday, July 20, 2024

Karia: Haya ni maandalizi ya Wafcon

 






RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Wallace Karia amesema maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya Wanawake (WAFCON) na michezo ya kalenda ya Fifa ni miongoni mwa sababu za kuipeleka Twiga Stars kushiriki michuano ya Kombe la Wanawake Tunisia.

Twiga Stars ilikuwa nchini Tunisia kuanzia Julai 9, mwaka huu ambako ilicheza michezo miwili mmoja dhidi ya Tunisia na kuifunga mabao 5-0 na Botswana ambao walitoka suluhu.
Akizungumza baada ya wachezaji hao kuwasili Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam leo, Karia alisema ushindi walioupata Twiga Stars kwenye mashindano ya Kombe la Tunisia utawasaidia kufanya vizuri kwenye Wafcon itakayofanyika nchini Morocco mwakani.

"Mashindano hayo yalikuwa ni maandalizi kuelekea mashindano ya Wafcon ambayo yatafanyika mwakani kwani malengo yetu ni kuona timu inakwenda kushindana na si kushiriki,” alisema Karia.

Rais huyo alisema wameamua kuitumia kalenda ya Fifa ili benchi la ufundi lihakikishe linaunda timu yenye ushindani katika mashindano hayo.

Naye Kocha Mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime alisema amefurahishwa na viwango vilivyooneshwa na wachezaji wake katika mashindano hayo na kudai walikwenda kwa lengo la kutwaa kombe hilo.

Alisema kuelekea kwenye mashindano ya Wafcon watakaa na kuzungumza na TFF kwa ajili ya kurekebisha mapungufu yao na changamoto kuhakikisha wanakwenda kufanya vema nchini Morocco.

"Tumefurahishwa na mafanikio haya na tumetumia kalenda ya Fifa kwa kucheza michezo mfululizo itakayotusaidia kufanya vizuri kwenye Wafcon,” alisema Shime.

Nahodha wa timu hiyo, Anastazia Katunzi alisema ushindi huo utawasaidia kuipeperusha vema bendera ya Tanzania na kuwataka Watanzania waendelee kuwaamini kwa kuwa malengo yao ni kufika mbali.

No comments:

Post a Comment