Pages

Saturday, July 20, 2024

APR, Red Arrows fainali Cecafa

 

Red Arrows

Kikosi cha APR

TIMU za APR ya Rwanda na Red Arrows ya Zambia leo zinatarajiwa kucheza fainali ya Kombe la Dar Port Kagame 2024 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, Tanzania.

Mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu utakuwa kati ya Al Hilal dhidi ya Al Wadi zote kutoka Sudan.

 Timu ya APR inayofundishwa na kocha Darko Novic iliiondoa Al Hilal kwa mikwaju ya penalti 5-4 katika nusu fainali ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC na Red Arrows ikaifunga Al Wadi FC ya Sudan kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi juzi.

 APR ambao wameshinda kombe hilo mara tatu walifuzu fainali bila kupoteza mchezo tangu hatua ya makundi lakini mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Zambia walipokea kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Al Hilal katika mechi za makundi.

 Kocha wa APR, Novic alisema anajivunia wachezaji wake ambao wana ari ya kupambana tangu mwanzo hadi kufuzu kwa fainali.

 "Bado tuna kazi kubwa ya kufanya kwa sababu maandalizi ya fainali ni tofauti hasa baada ya kucheza dakika 120 katika nusu fainali," alisema Novic.

 Naye mchezaji wa Red Arrows, Allasane Diarra ambaye alinyakua tuzo ya mchezaji bora wa mechi alisema hawakukata tamaa tangu mwanzo hadi mwisho.

 "Hii haikuwa mechi rahisi, lakini tulicheza kwa mioyo yetu na kufika fainali," alisema Diarra.

 Katika michuano hiyo ambayo itamalizika leo, mabingwa watajinyakulia zawadi ya fedha taslimu dola za Marekani 30,000 (Sh milioni 78), mshindi wa pili dola za Marekani 20,000 (Sh milioni 52) na mshindi wa tatu dola za Marekani 10,000 (Sh milioni 26).

 

No comments:

Post a Comment