Pages

Saturday, July 20, 2024

Kesi ya Yanga kuanza kusikilizwa upya

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imekubali ombi la Klabu ya Yanga la kusogezwa mbele kwa muda wa kusikilizwa kesi iliyofunguliwa na wanachama wa klabu hiyo kuhusu uhalali wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo.

Awali mahakama hiyo iliamuru Uongozi wa Yanga ukiongozwa na Rais Hersi Saidi kuachia ngazi kwa kile kilichodaiwa kuwa Katiba ya Yanga haitambui uwepo wao.

Kufuatia hatua hiyo mahakama hiyo imewapa siku 14 kama walivyoomba Yanga kufanya mapitio kisha kesi itasikilizwa upya kukiwa na pande zote mbili.

Hivi karibuni Yanga walipokea hukumu ya kutotambulika kwa Baraza la Wadhamini la klabu hiyo kutokana na hukumu iliyotolewa Agosti 2, 2023 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga, Wakili Simon Patrick alisema Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ilisikiliza kesi hiyo iliyofunguliwa na Juma Ali na Geofrey Mwaipopo upande mmoja kwani klabu haikushirikishwa.

Alisema Abeid aliwasilisha utetezi ambao saini za klabu zilighushiwa akidai wamemteua kwenye kesi hiyo mbele ya Hakimu Mwandamizi Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Pamela Mazengo.

Alisema Juma Ali na Geofrey Mwaipopo ambao walikuwa upande wa walalamikaji na Juma Abeid alikuwa upande wa Yanga (walalamikiwa) alikuwa akikubali kila kitu kilichokuwa kinaombwa na upande wa walalamikaji.

Baada ya hapo jopo la wanasheria wa Yanga walipeleka maombi mahakamani kuomba kuongezewa muda kwa ajili ya kufanya mapitio kwani muda wa kukata rufaa umeshapita na kukubaliwa.

Hukumu hiyo ilitokana na kesi ya msingi iliyofunguliwa Agosti 4, 2022 na walalamikaji Ally na Mwaipopo wakitaka kutotambulika kwa Baraza la Wadhamini la Yanga lililowekwa madarakani kwa katiba ya mwaka 2010, kukosa sifa kisheria.

Aidha, walalamikaji pia walitaka miamala yote ya fedha iliyoidhinishwa na baraza hilo, kutotambulika kisheria kwa kuwa ni batili.

Hukumu hiyo imeitaka bodi iliyokuwa madarakani kwa katiba ya mwaka 1968 iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2011, kurudi madarakani kuongoza klabu ya Yanga.

Inaelezwa kuwa walalamikaji walirudi mahakamani kukazia hukumu hiyo kuiondoa madarakani bodi hiyo ya wadhamini ndipo uongozi wa sasa wa Yanga ukapenyezewa taarifa.

Baraza lililolamikiwa linaongozwa na Mwenyekiti George Mkuchika na wajumbe ni mama Fatma Karume, Dk Mwigulu Nchemba, Tarimba Abbas na Antony Mavunde.

No comments:

Post a Comment