Pages

Tuesday, May 8, 2018

WAWILI WAONGEZWA NGORONGORO HEROES, KABWILI NJE


KOCHA wa timu ya taifa ya vijana waliochini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, Ammy Ninje ameongeza wachezaji wawili kwenye kikosi hicho akiwemo kipa Peter Doto na Nasry Daudi
Nasry Daudi anatoka Aspire ya Senegal na Doto anayeziba pengo la Ramadhan Kabwili anayecheza Yanga anatoka timu ya Black Sailor ya Zanzibar
Akizungumza jana Ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, Cliford Ndimbo alisema Doto ameshaingia kambini na Nasry alitarajiwa kuwasili usiku.
“Doto tayari yupo kambini lakini Nasry anatarajiwa kuwasili leo usiku (jana) kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa raundi ya pili ya mchujo wa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa dhidi ya Mali utakaochezwa Jumapili Uwanja wa Taifa,” alisema Ndimbo
Ngorongoro imefuzu hatua ya pili baada ya kuitoa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika raundi ya kwanza kwa penalti 6-5 mjini Kinshasa baada ya sare mbili za 0-0 nyumbani na ugenini.
Katika mechi zote Kabwili akidaka na baadae akaruhusiwa kwenda kwenye timu yake kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba uliochezwa Aprili 29 lakini hakurejea tena kambini badala yake aliungana na timu yake kwenda Algeria.
Kitendo cha kuondoka na timu yake kilimkasirisha kocha Ninje na kudai ni utovu wa nidhamu na kusema hatamhitaji tena bali atateua mchezaji mwingine kuziba nafasi yake
Kabwili alianza kuidakia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za U-17 za Afrika nchini Gabon Mei mwaka jana, ambayo wachezaji wake wengi ndio wanaunda Ngorongoro kwa sasa.

No comments:

Post a Comment