Pages

Tuesday, May 8, 2018

MWAKYEMBE AMWAGIZA TENGA KUSIMAMIA VYAMA VYA MICHEZO KUHESHIMU MUDA WA KUKAA MADARAKANI


WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amewataka wajumbe wa baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuhakikishe vyama vya michezo vinaheshimu katiba zao kwa kuheshimu vipindi vya uongozi na kufanya uchaguzi muda unapofika.
Dk. Mwakyembe aliyasema hayo jana wakati akizindua baraza la 14 ambalo lilitangazwa Februari 9, 2018 ambalo linaongozwa na Mwenyekiti Leodgar Tenga likiwa na wajumbe sita pamoja na wajumbe wengine watatu ambao wanaingia kutokana na vyeo vyao serikalini.
“Mwenyekiti napenda kukupongeza wewe binafsi pamoja na wajumbe wote mlioteuliwa kuunda baraza la 14, vilevile ninampongeza  kwa dhati mwenyekiti na wajumbe wote waliokuwa katika baraza la kumi na tatu,” alisema.
 “Tumefanya uteuzi wa wajumbe kwa kuzingatia umakini na uwezo wenu kwa kila mmoja tukiwa na malengo ya kuongeza ufanisi wa chombo hiki muhimu katika usimamizi wa maendeleo ya michezo nchini hivyo mmeteuliwa ili kuleta mabadiliko katika Sekta ya maendeleo ya michezo,” aliongeza Dk. Mwakyembe.
Alisema baraza lihakikishe kuwa vyama vya michezo vinaheshimu katiba zao ikiwa ni pamoja na kufanya uchaguzi kwa muda kwa kufuata kanuni za vyama husika muda unapofika pia kuhakikishe viongozi hawabinafsishi na kuwavunja moyo wanachama wao.
Baraza hilo ambalo limeteuliwa na Waziri Dk Mwakyembe chini ya sheria ya BMT ya mwaka 1967 linaundwa na Leodgar Tenga ambaye ni Mwenyekiti.
Wajumbe ni Profesa Mkumbwa Mtambo, Beatrice Singano, Kanali Mstaaafu Juma Ikangaa, John Ndumbaro, Rehema Madenge na Salmin Kaniki.
Wengine ambao wameingia kwa nafsi za vyeo vyao ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Yusuph Singo, Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Dk. Edicome Shirima na Katibu wa BMT, Mohamed Kiganja.


No comments:

Post a Comment