Pages

Sunday, May 13, 2018

NGORONGORO HEROES KATIKA KIBARUA KIGUMU UGENINI NA MALI





PAMOJA na kufungwa mabao 2-1 na Mali, timu ya taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes bado inaweza kusonga mbele katika kufuzu kwa mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa umri huo, Afcon endapo itachanga vizuri karata zao katika mchezo wa marudiano.
Baada ya kufungwa 2-1 katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili wa kufuzu kwa Afcon leo kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, Ngorongoro Heroes sasa inahitaji ushindi wa angalau mabao 2-0 ili kusonga mbele.
Timu hiyo iliitoa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa penalti 6-5 baada ya kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaama na baadae kupata matokeo kama hayo nchini Congo kabla ya kwenda katika matuta.
Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, umeifanya Ngorongoro kuwa na kibarua kigumu katika mchezo wa marudiano kwani sasa inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 ili kusonga mbele katika hatua inayofuata.
Mchezo huo ambao uliokuwa na ufundi mkubwa kwa timu zote mbili, timu ya Mali ilikuwa ya kwanza kuandika bao kupitia kwa kiungo Ousmane Diakite.
Wakati Ngorongoro ikicheza kwa juhudi zote kutafuta bao la kusawazisha,ndipo mshambuliaji Dianka wa Mali alipoipatia timu yake bao la pili kunako dakika ya 40.
Ngorongoro iliamka na kuanza kucheza kwa kasi ikitafuta bao, hata hivyo juhudi hizo zilianza kuzaa matunda baada ya mshambuliaji Paul Peter kufunga bao la kufutia machozi na kurudisha matumaini kwa Watanzania.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu na kujilinda zaidi ambapo mpaka dakika 90 zinamalizika matokeo yalibaki kwa Ngorongoro kupoteza kwa idadi hiyo ya mabao.

No comments:

Post a Comment