Pages

Sunday, May 13, 2018

YANGA NDIO KAMA MLIVYOSIKIA HUKO MORO


UPEPO mbaya umeendelea kuikumba klabu ya Yanga, baada ya leo kupoteza mchezo mwingine wa Ligi Kuu Bara kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Mchezo huo unakuwa ni wa tatu mfululizo kwa timu hiyo kupoteza, ikiwa kwenye viwanja tofauti baada ya ule wa Simba uliofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na Tanzania Prisons, uliofanyika Mbeya.
Katika mchezo huo ambao timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa zamu, huku Mtibwa ikijilinda zaidi kuepuka kupoteza mchezo huo.
Yanga ilijitahidi kufanya mashambulizi ya kushtukiza, lakini umakini mdogo wa washambuliaji, Yohana Nkomola na Matheo Anthony ulifanya mchezo huo kwenda mapumziko ukiwa sare ya bila kufungana.
Kipindi cha pili kilianza kwa Mtibwa kushambulia kwa mpira mirefu ambayo hata hivyo ilizimwa vizuri na walinzi wa pembeni, Juma Abdul na Salum Hassan.
Dakika ya 62  ilifanya mabadiliko ya kumtoa Juma Abdul ambaye aliumia na kuingia Yusufu Suleiman, ambaye hata hivyo alionekana kuwa na uzoefu mdogo wa Ligi.
Yanga ilicharuka na kuanza kupeleka mashambulizi kwa kutumia mipira mirefu, ambayo dakika ya 65 nusura wapate bao baada ya Thaban Kamusoko kugonga mwamba, kabla ya dakika nne baadaye Matheo Anthony kufanya hivyo pia.
Mtibwa ilionekana kudhamiria kuifunga Yanga, baada ya kufanya mabadiliko ya kumtoa Salum Kihimbwa na kuingia Haruna Chanongo ambaye alibadilisha taswira nzima ya mchezo huo kwa timu yake.
Wakati mchezo ukielekea ukingoni, kiungo Thabani Kamusoko alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Festo Simon, ambapo dakika moja baadaye mchezaji Hassan Dilunga aliipatia Mtibwa bao ambalo lilidumu hadi dakika 90 ya mchezo.
Baada ya mchezo huo, Yanga itaingia kambini kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Rayon Sports utakaopigwa Mei 16 wiki hii, kwenye dimba la Taifa,Dar es Ssalaa.
Kwa matokeo hayo, Yanga imeendelea kushika nafasi ya tatu kwa pointi 48, ikiwa nyuma ya Azam FC wenye pointi 52.
Yanga katika mchezo wa kwanza wa makundi wa Kombe la Shirikisho, ilifungwa mabao 4-0 na Alger Usm ya Algeria

No comments:

Post a Comment