*Wapo marais wanaosakata soka
hadi sasa
Monrovia (AFP) –
MWANASOKA bora wa zamani wa Dunia George Weah
ametangazwa kuwa rais wa Liberia baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa taifa hilo
alhamisi hii, akimpita kirahisi mpinzani wake Joseph Boakai.
"Wananchi wenzanngu wa Liberia, nahisi hisia za
taifa zima. Napima umuhimu wa
wajibu na majukumu yangu kwenu kwa ushindi huu.
Mabadiliko yanakuja,”alisema Weah kwenye akaunti yake ya Twitta.
Mamia ya mashabiki wake walikuwa wakizunguka kwenye
mitaa ya jiji la Monrovia kushanglia ushindi wa mwanasoka huyo nyota wa zamani
wa klabu za Monaco, Paris Saint-Germain, Ac Milan, Chelsea na Manchester City.
"Sikuwa na furaha kwenye maisha yangu yote.
Tulikuwa wapinzani kwa miaka 12.Tunaenda kuweka historia, kama ambavyo watoto
wa Afrika Kusini waliwahi kufanya.
Hivyo nina furaha sana," alisema Josephine
Davies, mgombea mwenza wa George Weah katika chama Congress for Democratic Change.
"Tulisubiri kwa miaka 12, sasa nguvu inarudi kwa
wananchi."
Weah, mwenye umri wa miaka 51 anachukua nafasi ya Ellen Johnson Sirleaf, ambae aliiongoza
Liberia tangu mwaka 2006.
Tume ya Uchaguzi ya taifa hilo ilisema Weah alishinda
kwa asilimia 61.5 ambapo matokeo hayo
yalicheleweshwa kwa wiki kadhaa akimshinda mpinzani wake Joseph Boakai.
Tume hiyo ya uchaguzi ilisema kati ya asilimia 98.1 ya
kula zote zilizohesabiwa, Boakai alipata asilimia 38.5.
UNAPOSIKIA majina ya wacheza
soka wa zamani kama vile Pele (Edson Arantes do Nascimento), Diego Maradona,
Zinedine Zidane au wa sasa Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Neymar na Mohamed
Salah, ujue kuna wengine wengi nyuma yao.
Hao ni pamoja na Rais mteule
wa Liberia, George Weah, ambaye baada ya safari ndefu ya milima na mabonde
kwenye siasa za nchi hiyo kwa zaidi ya muongo, na uchaguzi wa mwaka huu kuingia
raundi mbili, hatimaye ameukwaa urais.
Anaweka historia barani
Afrika kwa kuwa Rais wa kwanza aliyekuwa mwanasoka, na kwa namna ya pekee ni
mchezaji aliyepata kutwaa tuzo ya mwanasoka bora duniani, nayo ilikuwa 1995
akiwa wa kwanza kutoka Afrika kupewa tuzo hiyo – Ballon d’Or. Weah
alikuwa akikikipiga nafasi ya ushambuliaji na ni mmoja wa waliotokea kuwa
wakali zaidi wa zama zake.
Wakati mwaka 1989 na 1994
sawa na 1995 alichaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika, mwaka uliofuata
alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Afrika wa Karne. Alitambulika zaidi kwa kasi
yake ya kukokota mpira na ufungaji mabao bora kabisa. Shirikisho la Soka la
Kimataifa (Fifa) linamtaja kama mtu ambaye ingekuwa leo, basi angefanya kazi za
washambuliaji kadhaa.
Leo hii wapo viongozi wengine
wanaocheza soka, lakini si ile kali ya kiushindani, japokuwa nayo ni soka tu,
na wana pumzi ya kutosha. Nitawataja wawili, nao wanatoka Afrika Mashariki,
wakiwa ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi.
Sasa tuwaone watu waliocheza soka kisha wakaja kuwa viongozi wakubwa kisiasa au
kidini, mmoja akawa kiongozi wa kanisa mojawapo dunia nzima.
PAPA YOHANA PAULO 11
Akiwa mvulana mdogo huko kwao
Wodowice, Poland, Karol Jozef Wojtyla, alikuwa mchezaji mzuri wa soka katika
klabu yao ndogo ya shule na kidini. Huyu ndiye aliyekuja kuwa Kiongozi wa
Kanisa Katoliki Duniani, Papa Yohana Paulo II ambaye amefariki dunia na tayari
ametangazwa kuwa Mtakatifu.
Huyu amepata kudumisha amani
baina ya timu za jamii tofauti, akijitolea kucheza upande wa Wayahudi, pale
walipokuwa wakicheza dhidi ya Wakatoliki na ikatokea kwamba Wayahudi hawakuwa
na idadi ya kutosha ya wachezaji. Licha ya kufuata wito wa upadre na kupanda
hadi kuwa Baba Mtakatifu, Yohana Paulo II alibaki na mapendo kwa soka na huko
Brazil kuna uwanja unaitwa kwa jina lake - Estádio João Paulo II.
EVO MORALES
Evo Morales ni nani? Ndiye
Rais wa sasa wa Bolivia aliyecheza sana soka enzi zake. Akiwa na umri wa miaka
14, Morales alionesha ukomavu wa kiuongozi baada ya kuandaa kundi la wanasoka,
akawa kocha wao na mchezaji pia, na kikosi kikawa kizuri chenye ushindani
mkubwa kilichocheza kwenye jimbo zima analotoka.
Akiwa na umri wa miaka 16,
Morales alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa ufundi wa kikosi hicho kilichoingia
katika ligi ndogo ya eneo lao, na mwaka 1981 akiwa na umri wa miaka 22
alichaguliwa kuwa rais wa chama cha soka cha eneo lao.
Japokuwa Morales aliamua
kufuasa siasa na kujitolea kwa kile anachokiita kuboresha maisha ya watu wake,
anaendelea kucheza soka kila akipata nafasi popote pale nchini mwake. Jamaa
huyu aliyetokea kuwa pia mjumbe wa chama cha wafanyakazi mwenye siasa za mrengo
wa kushoto, anaipenda soka na hupenda kuwezesha watu kuicheza.
FERNANDO DE MELLO
Fernando Collor de Mello
alihudumu kama rais wa 32 wa Brazil. Alitumikia Ikulu kwa miaka miwili,
akajiuzulu 1992 kama njia mojawapo ya kukwepa kushitakiwa akiwa madarakani,
mashitaka yaliyokuwa yameletwa dhidi yake na serikali ya taifa lake.
Huyu alikuwa Rais wa kwanza
kuchaguliwa kwa uhuru na demokrasia ya uwazi baada ya kipindi cha utawala wa
kijeshi. De Mello alicheza soka sana muda wote wa ujana wake na akatumia soka
kama jukwaa lake au manati ya kumfanikishia mambo ya siasa.
Akiwa na umri wa miaka 27 tu,
De Mello alikuwa rais wa klabu ya Centro Sportivo Alagoano, akatumia umaarufu
aliojikusanyia kuwania na kutwaa nafasi ya meya wa Jimbo la Alagoas. Kwa sasa
si mtu anayeenziwa sana nchini Brazil, kwa sababu alichaguliwa kwa ajili ya
kudhibiti rushwa, lakini anadaiwa badala yake aliungana na wala rushwa, kama si
kuwazidi kwa kuila badala ya kuimaliza.
OSAMA BIN LADEN
Kiongozi wa zamani wa genge
la kigaidi la Al Qaeda, Osama Bin Laden ni mtu aliyekuwa na mahaba makubwa na
soka, akijadiliwa kwamba alikuwa shabiki mkubwa wa Arsenal, lakini haikuwa tu
imeelezwa kama alicheza. Sasa chukulia kwamba alicheza enzi za utoto na ujana
wake.
Hakucheza soka ya kulipwa
bali ile ya ridhaa, akawa huko sana, na inaelezwa kwamba ni kutoka huko
aliwachagua makamarada wake kwa ajili ya mambo yake ya kupigania aliyoyaamini
baadaye, akiwapeleka nje ya nchi.
BOB MARLEY
Bob Marley hakuna
kumfyatua Mzungu ubavuni, hakuna kumfyatua Mwafrika ubavuni, bali yeye
aliufyatua mpira huko uwanjani. Bob alikua akicheza soka nchini Jamaica akiwa
shule lakini pia nje ya shule katika ligi za mikoa na majimbo yao.
Baba yake alikuwa Mwingereza
na mama Mjamaica, akasema soka ilikuwa kwenye damu yake, lakini baadaye
akajikita zaidi kwenye muziki, japo kuna video zake za muziki akicheza soka pia.
Alibobea kwenye muziki kwas ababu enzi zile hapakuwapo fursa za kucheza soka ya
kulipwa huko Caribbean. Zipo picha nyingi mithili ya mabango, ya Bob, akicheza
soka, hata kwenye migahawa Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Arusha.
No comments:
Post a Comment