Pages

Wednesday, October 4, 2017

BASATA YAPONGEZA WAANDAJI WA MISS UNIVERSE

Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa na Masoko wa Basata, Vivian Shalua (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Miss Univerese mwaka jana, Jihan Dimachk (Kulia) na Miss Earth Tanzania, Lilian Loth.

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limeipongeza kampuni ya Compass Communications Tanzania kwa kufanya mashindano bora ya Miss Universe hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa na Masoko wa Basata, Vivian Shalua wakati wa kufanya tathimini ya mashindano hayo na mashindano ya urembo kwa ujumla.
Mrembo Jihan Dimachk alishinda taji la Miss Universe mwaka jana  huku Lilian Loth akishinda nafasi ya pili katika mashindano hayo.
Shalua alisema Basata wamefarijika sana na jinsi mashindano hayo yanavyoendeshwa na hakuna malalamiko yoyote kuhusiana na zawadi na upendeleo.
Alisema kuwa kutokana na utaratibu mzuri wa mashindano yao, Basata imeridhia waandaaji wa mashindano hayo, kufanya mashindano ya mwaka huu na vile vile kuandaa mashindano ya kutimiza miaka 10 tokea kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2007.
“Pamoja na kuwa na shindano moja kwa kushirikisha warembo wa mikoa tofauti, bado Basata imefarijika na jinsi mnavyoendesha na utaratibu unaotumia kuwapata warembo, uendeshaji wa mashindano mpaka kumpata mshindi,” 
“Tunajua kuwa kuna changamoto za wadhamini na kusababisha kufanya mashindano yenye kalenda fupi na kuondoa mlolongo wa matukio, hatua hii ni bora zaidi ili kuondoa malalamiko ya zawadi na mambo mengine, huu ni mfano wa kuigwa,” alisema Shalua.
Mkurugenzi wa Compass Communications ambaye pia ndiye mwandaaji mkuu wa mashindano haya Maria Sarungi Tsehai aliishukuru Basata kwa usimamiaji bora wa mashindano katika sekta ya sanaa nchini na kusema kuwa watajihidi kuongeza wigo ili kuona warembo wengi zaidi kutoka mikoa tofauti wanashiriki katika mashindano yao.
Maria alisema kuwa pamoja na changamoto zote wanazokabiliana nazo, bado wanahitaji msaada kutoka Basata ili kupata wadhamini na kufikia malengo yao katika kuendeleza Sanaa hapa nchini.
“Kwa sasa kuna changamoto kubwa ya wadhamini wa mashindano, kuna haja ya kupata msaada kutoka Basata ambao ni chombo cha serikali, mnaweza kutusaidia kupata wadhamini hata kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, sisi tunatangaza jina la nchi na utalii pia, tunaamini kupitia kwenu, tunaweza kupata sapoti kubwa kutoka wizara hiyo, Bodi ya Utalii (TTB) na mamlaka ya zake kama Tanapa,” alisema Maria.


No comments:

Post a Comment