Pages

Saturday, September 16, 2017

YANGA YATOKA SARE NA MAJIMAJI SONGEA LEO



MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga jana walipambana na hali yao baada ya kutoka nyuma na kulazimisha sare ya 1-1 na Majimaji katika mchezo uliofanyika mjini Songea.
Yanga wamelalamikia Uwanja wa Majimaji kuwa ndiyo umesabaisha timu yao kutocheza vizuri na kusababisha kuambulia sare hiyo katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alilalamikia uwanja huo na kusema kuwa umechangia kutopata ushindi, lakini aliipongeza Majimaji kwa sare hiyo.
Kocha wa Majimaji, Peter Mhina amewapongeza wachezaji wake na kusema kuwa walicheza vizuri huku akisema bao la Yanga lilipatikana baada ya mabeki wake kufanya makosa ya uzuiaji.
Mzimbabwe Donald Ngoma ndiye aliyeiokoa Yanga isiondoke na kichapo baada ya kufunga bao la kusawazisha katika katika dakika ya 79 kwa kichwa akimalizia krosi ya Mzambia, Obrey Chirwa.
Majimaji ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Peter Mapunda katika dakika ya 54 akimalizia pasi ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Jerry Tegete na kumfunga kipa Mcameroon, Youthe Rostand.
Kipindi cha kwanza wenyeji Majimaji walitawala mchezo na kufika mara nyingi kwenye eneo la hatari la Yanga, lakini hawakuweza kufunga.
Mchezo huo ulisimama kwa muda katika dakika ya 39 baada ya Emmanuel Martin wa Yanga kuzimia uwanjani baada ya kugongana na mchezaji wa Majimaji Mpoki Mwakinyuke.
Kwa sare hiyo Yanga imefikisha jumla ya pointi tano baada ya kucheza mechi tatu, baada ya kutoka sare mara mbili na kushinda mchezo mmoja huku Majimaji wakifikisha pointi mbili baada ya kufungwa mechi moja na sare mbili.
Kikosi cha Majimaji kilikuwa; Andrew Ntala, Juma Salamba, Mpoki Mwakinyuke, Kennedy Kipepe, Tumba Sued, Hassan Hamisi, Suleiman Kassim, Yakubu Kibiga/Abdulhalim Humud, Danny Mrwanda/Jerry Tegete, Marcel Kaheza na Peter Mapunda.
Yanga; Youthe Rostand, Juma Abdul/Hassan Kessy, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Kevin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa, Raphael Daudi, Donald Ngoma, Ibrahim Hajib na Geoffrey Mwashiuya/Eammnuel Martin/Said Juma.


No comments:

Post a Comment