Pages

Saturday, September 16, 2017

KAGERA SUGAR MECHI TATU, POINTI MOJA. MAXIME ASEMA LIGI BADO MBICHI



KAGERA Sugar imecheza mechi tatu  bila kupata ushindi tangu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya juzi kupokea kipigi cha bao 1-0 toka kwa Azam FC uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Katika mchezo wa ufunguzi uliochezwa uwanja wa Kaitaba, Agosti 26, Kagera Sugar walifungwa na Mbao FC 1-0 na mchezo uliofuata wakatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting.
Kocha wa timu hiyo Mecky Maxime alisema bado ana matumaini ya kufanya vizuri na yupo kwenye mbio za kuwania ubingwa kwani hajakata tamaa kwani timu yake ilicheza vizuri kuliko wapinzani wao Azam FC
“Tumepoteza mchezo wetu lakini nawapongeza wachezaji licha ya kufungwa bado waliendelea kucheza vizuri. Hii ni ligi bado tuna nafasi ya kufanya vizuri na kushinda na hatimaye kutwaa ubingwa.”
“Msimu uliooita tulianza kwa kufanya vibaya karibu mechi nne za kwanza lakini msimu huu hatutaki iwe hivyo. Nawaamini wachezaji watafanya vizuri, matokeo mabaya waniachie mimi wao waendelee kucheza uwanjani,” alisema Maxime
Pia Maxime alisema wanahukumiwa kwa matokeo pekee lakini walicheza vizuri muda mrefu, kosa moja wapinzani wakalitumia, wakafunga, wanajipanga kwa mechi zijazo ili wafanye vizuri.
Naye kocha msaidizi wa Azam, Idd Cheche alisema ushindi waliopata ulikuwa mgumu kwani Kagera walicheza vizuri ila wao walitumia nafasi moja waliyoipata kujihakikishia ushindi.
“Haikuwa mechi rahisi, wapinzani walifanya vizuri tumepata nafasi moja tumeitumia kupata pointi tatu nyumbani ni jambo la kumshukuru Mungu,” alisema Cheche.
Kwa ushindi huo Azam imefikisha pointi saba baada ya kucheza mechi tatu na kufunga mabao mawili huku nyavu zao zikiwa hazijaguswa.

No comments:

Post a Comment