Pages

Wednesday, September 6, 2017

BUSWITA KUANZA KUCHEZA YANGA AKIMALIZA KUILIPA SIMBA





KAMATI ya Sheria Katiba na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesema kiungo wa Yanga, Pius Buswita anaruhusiwa kucheza baada ya kuilipa Simba sh milioni 11.
Buswita alifungiwa mwaka mmoja baada ya Simba kumshitaki mchezaji huyo kwa kamati hiyo kwa madai ya kuingia makubaliano na klabu hiyo lakini baadae akasajiliwa na Yanga.
Akizungumza na wandishi wa habari leo Mwenyekiti wa kamati hiyo Wakili Elius Mwanjala alisema kwa sababu lengo la kamati yao ni kuona mpira unachezwa wameamua kumfungulia Buswita baada ya makubaliano ya pande tatu ambayo Simba, Yanga na mchezaji mwenyewe.
“Yanga wamekubali kuilipa Simba pesa zao kwani mchezaji mwenyewe amekiri kupokea pesa kutoka Simba na baada ya kulipwa pesa zote na kamati kujiridhisha kweli zimelipwa ndipo ataruhusiwa kucheza,” alisema Wakili Mwanjala.
Alisema kamati yao imetumia busara katika kumaliza shauri hilo ili kumpa nafasi mchezaji huyo na aweze kulinda kiwango chake kwani anaweza kuwa mchezaji wa timu ya Taifa kwani mchezaji huyo angeendelea kutumikia adhabu hiyo Simba na Yanga ndizo zingepata hasara kwani amechukua pesa pande zote mbili.
Aidha alisema Simba ingeweza kupeleka shauri hilo katika mahakama za kiraia kudai haki yao kwa sababu mchezaji huyo alisaini wakati wa kuchukua pesa hizo shilingi milioni 10 pamoja na gharama ya tiketi za ndege ambayo ni shilingi milioni moja zilizotajwa na Simba kwenye barua yao waliyoiwasilisha TFF.
Wakili Mwanjala alisema kamati imetoa onyo kali la kimaandishi kwa mchezaji huyo pia wameagiza timu zote kuwalipa wachezaji pesa za usajili (sign fee) mapema iwezekanavyo na endapo mchezaji atakuwa hajalipwa anatakiwa kuwasilisha malalamiko yake ili zikatwe kwenye malipo ya klabu.
Buswita alijiunga na Yanga akitokea Mbao FC ya Mwanza alifungiwa na kamati hiyo baada ya kusajiliwa na Yanga huku pia akiwa amesaini mkataba na Simba.

No comments:

Post a Comment