Pages

Sunday, June 25, 2017

NYAMLANI AJITOA KWENYE UCHAGUZI TFF NA LIPULI KUFANYA UCHAGUZI AGOSTI 5



 Image result for NYAMLANI
MGOMBEA wa Urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athumani Nyamlani amejitoa kwenye kinyang’anyiro katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 12 mwaka huu mjini Dodoma.
Nyamlani ambaye amewahi kuwa Makamu wa Rais wa TFF aliwasilisha barua jana ikiwa ni siku moja tu tangu Kamati ya Uchaguzi ipitishe jina lake kuwa miongoni mwa wagombea 10 wanaowania nafasi hiyo kwa sababu ni masuala binafsi.
Akizungumza na gazeti hili, Ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas alisema baada ya Nyamlani kujiaondoa wagombea wanaobaki tisa kwenye kinyang’anyiro ambao watahitajika kufika kwenye usaili Juni 29.
“Baada ya Nyamlani kujiondoa sasa wagombea wanaobaki ni Jamal Malinzi, Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Fredrick Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe,” alisema Lucas.
Mbali na Nyamlani kujitoa, mgombea wa nafasi ya Kamati ya Utendaji TFF, kutoka kanda ya Kagera na Geita, Abdallah Mussa aliondolewa kwa sababu ya kutoambatanisha kivuli cha cheti ya elimu ya sekondari.
Jumla ya wagombea 74 waliomba kuwania nafasi mbalimbali hivyo sasa wamebaki wagombea 72, urais ukiwa na wagombea tisa, Makamu wa Rais sita na wajumbe wa kamati ya utendaji 58.
Wakati huo huo kamati ya Uchaguzi ya TFF imesema uchaguzi wa klabu ya Lipuli ya Iringa utafanyika Agosti 5, na utasimamiwa na kamati hiyo.
Awali uchaguzi huo ulikuwa ufanyike Mei 29 lakini baada ya kamati kufuatilia taratibu mbalimbali, kanuni na sheria na kujirisha sasa mchakato huo utaanza kesho.
Tayari Kamati ya Uchaguzi ya TFF iko Iringa kwa ajili ya kutangaza rasmi uchaguzi huo ambako zoezi la kuchukua na kurejesha fomu litaanza Juni 28, mwaka huu.


No comments:

Post a Comment