Pages

Sunday, June 25, 2017

MTAA WA VICTOR WANYAMA WAYEYUKA, KIBAO CHAONDOLEWA




UONGOZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo umetengua mpango wa kumpa mtaa mchezaji wa Tottenham ya England, Victor Wanyama.
Akizungumza na gazeti hili Ofisa Uhusiano wa Ubungo, Bonwell Kapinga alisema majina ya mitaa hupendekezwa na kamati za mitaa husika kisha hupelekwa kwenye vikao vya kata (WDC) halafu maamuzi ya WDC hupelekwa kwa Mkurugenzi kwa ajili ya kuingizwa kwenye kikao Cha kamati ya Fedha na uongozi, Baraza la Madiwani, halafu DCC,  RCC na kisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na baadaye kwa mchapaji mkuu wa serikali na mwisho hutokea kwenye Tangazo la serikali GN. 
“ Baada ya taratibu hizo ndipo mtaa hujulikana huo ni mtaa fulani pia taratibu za kubadili pia lazima zifuate hatua hizo muhimu,” alisema Kapinga.
Kapinga alisema kilichofanyika ni kinyume na utaratibu wa kisheria ndio maana hicho kibao chenye jina hilo lilolowekwa jana kimeondolewa taratibu zifuatwe.
Wanyama alizaliwa Juni 25, 1991 alisoma shule ya Kamukunji  na kisoka aliibukia akademi ya JMJ kwao, kabla ya kuchezea Nairobi City Stars na AFC Leopards katika Ligi Kuu ya Kenya.
Mwaka 2007 alijiunga na Allsvenskan ya Helsingborg nchini Sweden, lakini akalazimika kuondoka baada ya kaka yake, McDonald Mariga kwenda Parma ya Italia mwaka 2008 na Wanyama akarejea Kenya.
Baadaye alikwenda kufanya majaribio Beerschot AC ya Ubelgiji na kufuzu na kusaini mkataba wa miaka wa minne kuanza kucheza rasmi Ulaya mwaka 2008, kabla ya mwaka 2011 kununuliwa na Celtic ya Ligi Kuu ya Scotland.
Mwaka 2013 alinunuliwa na Southampton ya England kwa dau la Pauni Milioni 12.5 na kuwa Mkenya wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England. Baada ya mechi 85 akifunga mabao manne, Wanyama akanunuliwa na Tottenham Hotspur mwaka jana kwa dau la Pauni Milioni 11 na msimu huu ameiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu, nyuma ya Chelsea walioibuka mabingwa.


No comments:

Post a Comment