Pages

Sunday, June 25, 2017

KICHUYA AIPA TAIFA STARS USHINDI COSAFA



 http://images.performgroup.com/di/library/Goal_Tanzania/36/2c/azam-vs-simba_oamaf9huq6c01mt0zougjygje.png?t=1026452143&w=620&h=430
TANZANIA imeanza vyema michuano ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA) baada ya kushinda mabao 2-0 kwenye mchezo wa Kundi A dhidi ya Malawi leo katika Uwanja wa Moruleng Afrika Kusini.
Shiza Kichuya alifunga mabao yote ya Taifa Stars kipindi cha kwanza, dakika ya 13 na 18.
Mabao ya Kichuya, mshindi wa tuzo ya Bao Bora Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, yanamfanya kocha Salum Shaaban Mayanga aandike ushindi wa tatu katika mechi nne tangu aanze kuifundisha Taifa Stars Machi mwaka huu, akimpokea Mtanzania mwenzake, Charles Boniface Mkwasa.
Tanzania kutoka Mashariki mwa Afrika, inashiriki kama mwalikwa ikiwa mara ya tatu ipo Kundi A na Malawi, Mauritius na Angola zinazomenyana kuanzia Saa 12:00 jioni hii hapo hapo Moruleng.
 Kundi B lina timu za Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe na mshindi wa kwanza wa kila kundi atakwenda moja kwa moja hatua ya Robo Fainali. Botswana, Zambia na Afrika Kusini, Namibia, Lesotho na Swaziland zimefuzu moja kwa moja Robo Fainali.
Kocha Mayanga anaitumia michuano hii kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wake wa kwanza wa kufuzu Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
Taifa Stars itaanza na Rwanda, mchezo wa kwanza ukichezwa Julai 15 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, kabla ya kurudiana mjini Kigali Julai 21, mwaka huu.
Kikosi cha Tanzania leo kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe/Hassan Kessy, Gardiel Michael, Abdi Banda, Saalim Mbonde, Erasto Nyoni, Himid Mao, Shiza Kichuya, Simon Msuva, Muzamil Yasssin, Elias Maguri/Mbaraka Yussuf dk62.

No comments:

Post a Comment